Wizara ya Afya nchini Kenya inasema nchi imeimarisha juhudi za kinga baada ya Tanzania kutangaza kuwepo kwa maambukizi ya ugonjwa wa Marburg,
"Lazima tuwe waangalifu na kujiandaa," Dkt. Patrick Amoth, Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Afya alisema,
Kenya na Tanzania zinapakana na watu wengi husafiri na kufanya biashara kati ya nchi hizi mbili kila siku.
Hakuna maambukizi yoyote ya Marburg yaliyoripotiwa nchini Kenya lakini nchi hiyo inakabiliana na ugonjwa mwingine wa Mpox.
Tanzania imeripoti jumla ya maambukizi 25 yanayoshukiwa kuwa Marburg.
Wizara ya Afya nchini Tanzania imethibitisha kuwa ni mtu mmoja tu amepatikana na ugonjwa huo.
Awali Tanzania iliripoti mlipuko wa kwanza wa Marburg Machi 2023, katika mkoa wa Kagera, ambapo jumla ya maambukizi tisa na vifo sita viliripotiwa, kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO).
Kulingana na Wizara ya Afya, Kenya imeweka utaratibu ikiwa ni pamoja na kuandaa Mpango wa Maandalizi na Kukabiliana na Ugonjwa wa Virusi vya Marburg, uchunguzi ulioimarishwa katika kaunti zote na maeneo ya mipakani, na tathmini ya kuangalia uwezo wa nchi wa kukabiliana na virusi hivyo.
Tanzania yaimarisha taratibu za afya
Wizara ya Afya ya Tanzania imetoa maelekezo ya kuzuia maambukizi mapya ya Marburg.
Wasafiri wote kutoka Kigera watatarajiwa kujaza fomu ya maelezo yao.
Wizara imesema yeyote atakayetambulika kuwa na uhusiano wa moja kwa moja na anayeshukiwa kuwa na ugonjwa wa Marburg itabidi awekwe kwenye uangalizi hadi pale madaktari watakapojiridhisha kuwa hana maradhi hayo.
Wanaosafiri kwa ndege, gari au vyombo vya kwenye maji watapimwa joto la mwili.