Mawaziri wa Fedha wa Kenya, Tanzania na Uganda wakionyesha bajeti za mwaka wa fedha 2024/2025.

Raia wa Afrika Mashariki, hasa kutoka Tanzania, Kenya, Uganda na Sudan Kusini, kwa mara nyengine, wanategea sikio leo hii ambapo nchi zao zinawasilisha Bajeti Kuu ya Serikali kwa ajili ya mwaka wa fedha 2024/25.

Waziri wa Fedha nchini Tanzania Mwigulu Nchemba, kwa niaba ya serikali ya nchi hiyo, atawasilisha bajeti ya shilingi trilioni 49.34, ambayo ni sawa na ongezeko la asimilia 11.2 ya bajeti ya mwaka 2023/2024 ambayo ilikuwa shilingi trilioni 44.3.

Kwa mujibu wa Wizara ya Fedha, asilimia 70.1 ya Bajeti Kuu inatarajiwa kutoka katika mapato ya ndani."Sehemu kubwa ya bajeti asilimia 70.1 itagharamiwa na mapato ya ndani ambayo yanatarajiwa kuongezeka kwa asilimia 10.0 mwaka 2024/25," alisema Nchemba.

Akinukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari nchini Tanzania,

Mwanadiplomasia na mchambuzi wa siasa, Hamduni Maliseli, amesema iwapo bajeti hiyo itatekelezwa kama ilivyokusudiwa, basi inaweza kuleta mapinduzi katika sekta mbalimbali ikiwamo kilimo, elimu na uwekezaji.

Waziri wa fedha wa Kenya  Profesa Njuguna Ndung'u akifika bungeni ytayari kusoma bajeti ya mwaka wa 2024/25 / Picha kutoka Bunge la Kenya 

Katika Bajeti hiyo, serikali pia imeainisha vipaombele vyake, ambapo imejikita zaidi katika mahitaji muhimu ikiwemo upatikanaji wa huduma muhimu kwa wananchi kama vile maji, umeme na miundombinu.

Kwa mujibu wa Wizara ya Fedha ya Tanzania, shilingi trilioni 15.78 zinatarajiwa kutumika kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.

Hata hivyo, Bajeti ya mwaka huu inasomwa wakati ambapo wananchi kutoka mataifa haya ya Afrika Mashariki, wamekuwa wakilalamikia ugumu wa maisha unaosababishwa na kupanda kwa gharama za bidhaa muhimu ikiwemo chakula.

Ni kutokana na hilo, ndio maana wananchi wa kada mbalimbali ikiwemo wanafanyabiashara wadogo na wakubwa, wamejawa na shauku kubwa ya kutaka kujua, iwapo mapendekezo ya bajeti ya mwaka huu yataleta afueni yoyote katika maisha yao ya kila siku.

Bajeti ya Kenya

Kwa upande wake, bajeti ya Kenya ya mwaka huu ni dola za kimarekani bilioni 36.7, ambapo katika mwaka wa fedha uliuopita, ilikuwa dola za kimarekani bilioni 28.5.

Serikali ya nchi hiyo inatarajia kukusanya dola bilioni 16.9 kutoka mapato ya ndani.

Hata hivyo, nchini Kenya, kumeshuhudiwa mjadala mkali kutoka kwa wananchi, ambao wamekuwa wakijaribu kutumia ushawishi wa mitandao ya kijamii kuwahimiza viongozi wao kupiga kura dhidi ya mswada wa fedha ambao ni sehemu ya bajeti kuu.

Miongoni mwa vipengele vya mswada huo ni pamoja na kuongezeka kwa kodi katika bidhaa kadhaa muhimu ikiwemo mafuta ya kupikia, mkate, na mawasiliano

“Katika hatua hii, kila anayeifanyia kampeni ni adui wa umma, asiyeipinga ni adui wa umma, yeyote atakayeipigia kura ni adui wa umma, yeyote atakayejizuia kupiga kura ni adui wa umma….tutawaangalia, msidhani kwamba mtakapo kaa kando bila kupiga kura mtakuwa mmesalimika,” amesema Fanya Mambo Kinuthia, mmoja wa wachambuzi wa masuala ya kisiasa nchini Kenya.

Waziri wa fedha Uganda Matia Kasaija anasoma bajeti yenye lengo la zaidi ya dola bilioni 19.3 kwa mwaka wa 2024/2025/ picha kutoka Bunge ya Uganda 

Katika hali ya kushangaza nchini Kenya, raia mmoja ameonekana akijaribu kuunyakua mkoba wa Waziri wa Fedha wa nchi hiyo ambao ulikuwa na Bajeti Kuu ya nchi. Hata hivyo, mwananchi huyo ameishia kutiwa mbaroni na vikosi vya ulinzi na usalama.

Bajeti Uganda

Uganda nayo inasoma bajeti ya dola bilioni 19.3. Hii ni ongezeko kutoka kwa dola bilioni 14.1 ambayo bajeti ya mwaka wa 2023/2024 ilitangaza.

Nchi hiyo imelenga kupata zaidi ya dola bilioni 8.6 kutoka kwa mapato ya ndani ya nchi .

TRT Afrika