John Dramani Mahama anaapishwa kwa muhula wake wa pili kama Rais wa Ghana / Picha: Reuters

Januari 7, John Dramani Mahama ameapishwa kama Rais wa Ghana, akijiandaa kuchukua hatamu ya uongozi wa nchi hiyo, kwa mara yake ya pili. Mahama anarejea Ikulu akiwa na jukumu kubwa la kukabiliana na changamoto mbalimbali ikiwemo ufisadi, ukosefu mkubwa wa ajira, mfumuko wa bei na kushuka kwa imani ya wananchi katika serikali ya nchi hiyo.

Kiongozi huyo wa upinzani, mwenye umri wa miaka 66, alishinda kiti cha urais katika uchaguzi wa Disemba 7, 2024, akirejea tena katika siasa ya nchi hiyo ambayo ni mzalishaji mkubwa wa pili wa zao la Kakao ulimwenguni.

Atakuwa akichukua nafasi ya Nana Akufo-Addo, ambaye anajiuzulu baada ya kuhudumu kwa mihula miwili, akiendeleza utaratibu wa kidemokrasia wa taifa hilo lililokumbwa na mapinduzi ya kijeshi na uasi wa magaidi.

John Dramani Mahama alishinda Uchaguzi wa Rais wa 7 Disemba 2024, kwa kura nyingi na kurejea katika ulingo wa kisiasa katika taifa hilo la Afrika Magharibi/ Picha: Reuters 

Taifa hilo lipo katika harakati ya kurejea katika hali yake ya kawaida kufuatia janga la Uviko19, kupanda kwa gharama za maisha na mzigo wa deni.

Lakini Mahama atakuwa chini ya shinikizo kutekeleza haraka ahadi za kampeni za kukabiliana na ukosefu mkubwa wa ajira kwa vijana na kupambana na rushwa iliyokita mizizi, hali inayopunguza imani ya raia kwa serikali ya nchi hiyo.

"Subira inazidi kupotea kwa raia wa kawaida wa nchi hii," anasema Godfred Bokpin, Profesa wa uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Ghana, katika mahojiano yake na Reuters.

"Licha ya wapiga kura kutimiza jukumu lao, bado wanajiuliza ni kipi wamekivuna kutokana na demokrasia hii?"

John Dramani Mahama anachukua nafasi ya Nana Akufo-Addo, ambaye anajiuzulu baada ya kuhudumu kwa mihula miwili/Picha: AA

Wachambuzi na wafuasi wa chama cha Mahama cha National Democratic Congress (NDC) wanaona uzoefu wake wa kisiasa na wingi wa theluthi mbili bungeni kama jukumu kubwa la kuchukua maamuzi magumu na kutekeleza sera za kuaminika za kuboresha maisha na kurejesha imani ya wawekezaji.

Mahama alikua Rais mwaka wa 2012 wakati John Evans Atta-Mills alipofariki akiwa madarakani.

Alishinda uchaguzi wa Urais miezi michache baadaye na muhula wake wa kwanza na wa pekee ulikumbwa na uhaba wa umeme, kuyumba kwa uchumi na madai ya ufisadi wa kisiasa.

Pata habari zaidi kupitia Whatsapp channels

TRT Afrika