Na Charles Mgbolu
Uwepo wa vichekesho vya mtandaoni umezua tofauti kubwa kutoka kwa muundo wa vichekesho vya kusimama wa kizazi cha kwanza, ambacho kilishuhudia wachekeshaji wakisimama mbele ya ukumbi uliojaa na kutoa vichekesho.
Katika kipindi cha miaka kumi hivi iliyopita, kumekuwa na mabadiliko makubwa, huku ufikiaji vichekesho ukiwa rahisi zaidi kutokana na teknolojia ya kidijitali.
Mtu akiwa tu na simu na intaneti alichobaki sasa ni kuchagua anataka kuona vichekesho gani mtandaoni.
Hii inaonekana katika idadi ya maoni yaliyorekodiwa mtandaoni.
Kwa mfano, mchekeshaji maarufu Nigeria Samuel Animashaun Perry ametazamwa na kama milioni nne katika video yake moja .
Data kutoka kwa Taasisi ya Africa Polling Institute (API) inaonyesha kuwa wasanii watano bora wa vichekesho kutoka Nigeria pekee wana wafuasi zaidi ya milioni 53 kwenye majukwaa mbalimbali ya mitandao ya kijamii.
‘’Hapa ndipo biashara ipo sasa ,’’ Christian Iroka, mtengenezaji wa vichekesho wa mtandaoni wa Nigeria, anaiambia TRT Afrika.
‘’Wafanyabiashara wengi wanapenda kufanya kazi na wale ambao wana wafuasi wengi kwenye mitandao ya kijamii. Ndio maana muundo huu mpya wa vichekesho unakua kwa kasi,’’ asema.
Yaga, mtayarishaji wa maudhui mtandaoni, ni Mkenya aliye na wafuasi zaidi ya milioni 1.2 kwenye TikTok. Anasema ucheshi wa kusimama hauna wafuasi wengi.
" Kwa vichekesho vya kusimama, una chumba hicho cha watu, vyovyote vile idadi yao, ndio pekee unaoweza kufikia na vicjhekesho yako kwa wakati huo,’’ alisema.
‘’Lakini kwa majukwaa ya mtandaoni, idadi ya watu unaweza kufikia haina mwisho, haina kikomo,’’ anaiambia TRT Afrika.
Katika miaka ya 1990 na 2000, vichekesho vya kusimama vilikuwa na biashara huku tikiti zikiuzwa kama halua moto.
Katika msimu wa likizo, tikiti za maonyesho ya vichekesho nchini Nigeria ziliuzwa kwa kiasi cha N1,000,000 ($1,250).
Lakini leo, matukio ya wachekeshaji wa kusimama si ya kawaida na sio maarufu.
"Muda mrefu umepita tangu niliposikia mara ya mwisho matukio kama haya yakifanyika,’’ asema Christian Iroka. ‘’Ni mabadiliko makubwa kutokana na baadhi ya wachekeshaji ambao sasa wanahamia kutengeneza maudhui ya mitandao ya kijamii,’’ alisema.
Mapato makubwa
Baadhi ya majukwaa ya mitandao ya kijamii, kama vile YouTube, huwalipa watengenezaji wa maudhui hadi $40,000 kwa mwezi.
Meta, baada ya kuzinduliwa kwa Facebook na Instagram Reels, inasema inawalipa waundaji hadi $35,000 kwa mwezi kulingana na maoni kwa vichekesho vyao.
"Matukio ya kuchekesha ya kusimama hayawezi kushindana na mapato haya. Ni aina gani ya vichekesho vya kusimama vinaweza kumlipa mcheshekeshaji aina hiyo ya pesa kila mwezi?’’ anauliza Yaga.
‘’Makampuni yatakutafuta unapokuwa na wafuasi wengi kwenye mitandao ya kijamii, kwa hivyo kusukuma maudhui yako zaidi kwenye mitandao ya kijamii ni faida kubwa,’’ asema Eric Omondi, mchekeshaji anayefuatiliwa zaidi na Kenya kwenye mitandao ya kijamii.
David Mensah, mchekeshaji wa kusimama kutoka Ghana, anaamini uigizaji wa ana kwa ana bado unafaa.
‘’Siku zote kutakuwa na watu wanaopenda na kuthamini uchekeshaji wa ana kwa ana. Wachekeshaji wa kusimama wanahitaji tu kujipanga upya na mikakati yao ya kibiashara,’’ anasema Mensah.
Wachekeshaji wengi wanaosimama wanajua wanahitaji kubadilika kulingana na wakati na sasa pia wanachapisha matukio yao ya kusimama kwenye majukwaa ya mitandao ya kijamii.
‘’Bado kuna tofauti kubwa kwa sababu wacheshekeshaji waliosimama huchapisha tu video baada ya kuandaa tukio, jambo ambalo huchukua miezi kadhaa kupangwa. Haiwezi kuwa sawa na mtayarishaji wa maudhui ya vichekesho mtandaoni ambaye wakati mwingine huchapisha video kila siku,’’ anasema Mensah.
Hali si rahisi waundaji wa maudhui ya vichekesho mtandaoni pia.
Hakuna kitu kizuri kinachokuja kwa urahisi, anasema Yaga.
''Lazima ufanye bidii kutengeneza nambari hizo mtandaoni na kupata maoni hayo. Binafsi niliambiwa na watu wangu wa karibu kwamba sikuwa mcheshi na kwamba nilikuwa nikipoteza wakati wangu, lakini sikuruhusu hilo kunikatisha tamaa,’’ aeleza.
Hatua ya kuelekea michezo ya vichekesho mtandaoni ni jambo la kuridhisha lakini watu hawatosheki.
Kwa hivyo wanapotamani ucheshi wa aina mbalimbali, labda wacheshi waliosimama watapata nafasi yao tena.