Jeshi la Kenya limetangaza mapema Jumatano kwamba vikosi vyake viliwaua wanamgambo sita wa Al Shabaab, akiwemo mpiganaji wa kigeni, wakati wa operesheni katika kaunti ya pwani ya Lamu.
Operesheni hiyo ililenga kundi la wanamgambo wa Al-Shabaab katika eneo kubwa la Msitu wa Boni. Miongoni mwa waliouawa ni pamoja na raia wa kigeni ambaye bado hajajulikana utambulisho wake.
"Operesheni hiyo ilifanikiwa kuwamaliza wanachama sita wa Al Shabaab, akiwemo raia wa kigeni, na kusababisha kutwaliwa kwa vifaa muhimu," KDF ilisema katika taarifa.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, uvamizi huo ulifanyika kufuatia taarifa za kijasusi kuwa kundi hilo lilikuwa linapanga mashambulizi katika eneo hilo.
KDF imesema baadhi ya magaidi hao walifanikiwa kutoroka na kuwashauri wananchi kuwa macho kwani huenda operesheni hiyo ikasababisha ongezeko la shughuli za kundi hilo hasa kwa vile idadi ya magaidi waliojeruhiwa inaripotiwa kuwa kubwa.
Al-Shabaab ni kundi la kigaidi lililokita kambi Somalia, ambalo limehusika na mashambulizi ya mara kwa mara nchini Kenya.