Sera ya Rwanda kupokea wahamiaji kutoka Uingereza imetupiliwa mbali. Rais Paul Kagame wa Rwanda na aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak walifanya makubaliano kuhusu suala hili.
Lakini miaka miwili baadaye bado utekelezaji wake haujafanyika baada ya kupata upinzani mkali hasa kutoka kwa wabunge wa Uingereza.
Waziri Mkuu mpya wa Uingereza naye ameongeza sauti kwa kusema kuwa mpango huo hautatekelezeka.
"Mpango wa Rwanda - mpango wa serikali iliyopita kutuma waomba hifadhi nchini Rwanda" ulikufa na kuzikwa kabla ya kuanza. Maana yake hatuendelei na mpango huo, bali mpango mbadala kuhusu uhamiaji," Waziri Mkuu Keir Starmer amesema.
Bunge ya Uingereza liliidhinisha sheria hiyo yenye utata mwezi Aprili, na kutangaza Rwanda kuwa nchi ya tatu salama. Hata hivyo, Mahakama ya Juu ya Uingereza ambayo ilikuwa ushatoa uamuzi kuwa mpango huo ni kinyume cha sheria kwa misingi ya haki za binadamu.
"Ni uamuzi unaokubalika sana - lakini kazi ya kujenga upya mfumo wetu wa hifadhi ili kukabiliana na changamoto za karne hii ni kubwa," Justin Welby askofu mkuu wa cantebury amesema.
Rais wa Rwanda amenukuliwa akisema hapo awali kuwa ikiwa mpango huo hautafaulu.
"Fedha hizo zitatumika kwa watu ambao watatumwa Rwanda," Rais Paul Kagame aliwaambia waandishi wa habari Januari mwaka huu.
"Ikiwa hawatakuja tunaweza kurudisha pesa hizo," Kagame alisema.
Gharama ya jumla ya kupeleka wahamiaji Rwanda ilikadiriwa kuwa karibu zaidi ya dola milioni 300 ambazo Rwanda imepokea.
Hii haihusishi gharama ya chakula na usafirishaji, malipo ya msimamizi na mahakama pamoja na safari za ndege.
Mamlaka ya Uingereza ilianza kuwazuia wanaotafuta hifadhi mwezi Mei.
Waziri Mkuu wa wakati huo Rishi Sunak, ambaye aliahidi kuwazuia wahamiaji na wanaotafuta hifadhi wanaofika kwa usafiri wa boti ndogo kutoka bara la Ulaya, alikuwa amesisitiza sera hiyo.
Serikali ya Rwanda bado haijatoa taarifa yoyote baada ya tamko la Waziri Mkuu mpya wa Uingereza.