Je, mkutano wa Al Burhan na rais Ruto utafungua maongezi ya amani Sudan?

Je, mkutano wa Al Burhan na rais Ruto utafungua maongezi ya amani Sudan?

Mkuu wa Jeshi la Sudan Al Burhan na rais wa Kenya William Ruto walikutana Kenya siku ya Jumatatu
Jenerali Al Burhan akutana na rais wa Kenya William Ruto jijini Nairobi. Picha/Ikulu Kenya

Ziara ya Mkuu wa Jeshi la Sudan na Kiongozi wa Baraza la Uongozi wa Mpito Jenerali Abdel-Fattah Al Burhan, nchini Kenya kwa ajili ya kukutana na rais wa nchi hiyo, William Ruto umeleta matumaini ya kuwepo kwa mazungumzo ya amani ya Sudan.

Vita nchini humo vilianza Aprili 15 mwaka huu.

"Viongozi hao wawili walisisitiza haja ya kuharakisha kutafuta suluhu ya mzozo wa Sudan haraka iwezekanavyo," Ikulu ya Kenya imesema katika taarifa.

Hata hivyo, ziara ya Jenerali Al Burhan inaangaliwa kama hali ya yeye kubadili msimamo wake kuhusu jukumu la Kenya kuwa mpatanishi kwa mzozo wa Sudan.

Mwezi Juni mwaka huu, Sudan ilikataa mwaliko wa Kenya wa mkutano wa Mamlaka ya Kiserikali ya Maendeleo (IGAD) kujadili mzozo wa Sudan.

Al Burhan akiwa na rais William Ruto wa Kenya. Picha/Ikulu ya Kenya

IGAD ilitangaza kuunda kamati inayoongozwa na Kenya na Sudan Kusini kutafuta suluhu ya mzozo wa Sudan. Ethiopia na Somalia ni wanachama wa kamati hiyo.

"Sudan bado inasubiri jibu kutoka kwa mamlaka ya kikanda ya IGAD kuhusu pingamizi lake la uenyekiti wa Kenya katika kundi la wapatanishi," Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan ilisema.

Jenerali Al Burhan alikataa uongozi wa Ruto katika upatanishi na kumtuhumu kuwa upande wa vikosi vya Rapid Support Forces (RSF). Jeshi la Sudan lilipendekeza juhudi hizo ziwe chini ya uongozi wa Rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir Mayardit.

Juhudi za amani zagonga mwamba

Saudi Arabia , Marekani na Umoja wa Afrika zimejaribu kufanya maongezi ya amani kwa ajili ya kuhimiza pande zinazozozana Sudan kusitisha mapigano, lakini hazijafua dafu.

Wananchi Sudan wanavuka mipaka kwenda nchi jirani ya Chad wakitoroka vita / Picha: Reuters 

Mwezi Mei Saudi Arabia na Marekani zilisaidia kupata mikataba mifupi ya kusitisha mapigano mwezi Mei kati ya pande zinazopigana.

Mazungumzo ya Jeddah yalifanyika tena Oktoba mwaka huu, yanayoongozwa na maafisa wa Saudi na Marekani.

Lakini vita vimeendelea

"Msiba unatokea mbele ya macho yetu nchini Sudan," Shirika la Umoja wa Mataifa la Kutetea Haki za Wakimbizi, UNHCR limesema, na kuongeza, "Maelfu wamepoteza maisha, watu milioni 6 wamepoteza makaazi yao. Imetosha. Vita lazima visitishwe."

"Takriban watu milioni 25 nchini Sudan sasa wanahitaji msaada wa kibinadamu," Martin Griffiths, mkuu wa huduma za kibinadamu za UN, alisema.

Mipango mipya ya amani

Ziara ya Jenerali Al Burhan nchini Kenya huenda ikafanya sasa majirani wa Sudan kuongoza mfumo wa upatanishi.

Mkutano wa viongozi hao wawili ulisema kasi ya mazungumzo ya Jeddah ni ndogo.

" Kwa kutambua kasi ndogo ya mazungumzo ya Jeddah, viongozi walisisitiza umuhimu wa kuharakisha mchakato wa kukomesha uhasama na kuharakisha usaidizi wa kibinadamu," taarifa kutoka Ikulu ya Nairobi imesema.

Wameamua mkutano wa dharua wa mamlaka ya IGAD uitwe kwa ajili ya "kutafuta njia za kuharakisha mchakato wa Jeddah na kusitisha mapigano nchini Sudan."

TRT Afrika