Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Maagizo ya Huduma kwa Jamii ya Kenya (NCSOC) Lilian Mutende anapendekeza kuachiliwa kwa wahalifu mwenye makosa madogo madogo ili kukabiliana na msongamano katika magereza ya Kenya.
Mutende, Jaji wa Mahakama Kuu, anasema kuwa msongamano wa sasa wa magereza unaweza kushughulikiwa ikiwa mfumo wa mahakama utarekebishwa ili kupitisha mbinu tofauti za adhabu kwa makosa madogo madogo.
“Msongamano ni wasiwasi mkubwa. Vituo vyetu vya marekebisho vilijengwa zamani sana, vyengine hata wakati wa ukoloni. Vimekarabatiwa na maeneo ya ziada kujengwa, lakini havitoshi kwa sababu ya ongezeko la watu,” alisema.
Alisema kwa sasa magereza ya Kenya yana takriban wafungwa 62,000 mara mbili ya uwezo wake ambao ni 30,000.
Rais William Ruto amekuwa akitaka hatua mbadala za kusuluhisha mizozo ya kufungwa jela kwa makosa madogo kwa sababu ya msongamano wa wafungwa.
Aprili 2023 mwaka jana, Rais alisema zaidi ya wafungwa 10,000 walikuwa wakitumikia vifungo vya chini ya miaka mitatu, na kwamba asilimia 41 ya wafungwa walikuwa wakisubiri kufikishwa mahakamani kwa makosa yanayoweza kudhaminiwa.
Wakati huo Waziri Mkuu alisema kuwa kupitia sera ya ‘Nguvu ya Rehema,’ serikali ilikusudia kupunguza msongamano wa magereza na vituo vyengine vya kurekebisha tabia kwa asilimia 50.