Kuna malalamiko 6 mbele ya mahakama ambayo yanapinga kuondolewa kwa Naibu Rais wa Kenya Rigathi Gachagua / Picha: Reuters

Jaji Mkuu nchini Kenya Martha Koome amewataja majaji watatu ili wasikilize kesi ya kutaka kuondolewa kwa Naibu Rais madarakani.

Erick Ogolla, Frida Mugambi na Anthony Mrima ndio waliotajwa kuwa katika benchi ya majaji watatu watakaosikiliza na kuamua kesi zilizounganishwa za kuondolewa kwa Naibu Rais Rigathi Gachagua.

Mahakama imepokea malalamiko sita ya kupinga mchakato wa kuondolewa kwa Naibu Rais Rigathi Gachagua.

Bunge la Taifa nchini Kenya Oktoba 8, 2024 lilipiga kura ya kumng’atua Naibu Rais wa Kenya, Rigathi Gachagua madarakani.

Gachagua ameshutumiwa kwa kukiuka katiba, kutomheshimu Rais na taasisi nyengine za serikali.

Wabunge 281 wamepiga kura ya ndio kuunga mkono hoja ya kuondolewa mamlakani, huku wengine 44 wakipinga kutolewa kwake.

Wiki iliyopita mawakili wanaomuakilisha Gachagua waliiambia Mahakama Kuu kuwa malalamiko yanayomkabili Gachagua ni mazito na yanahitaji timu maalumu kuyasikiliza.

Mahakama Kuu ilikubaliana na mawakili wa Gachagua wakiongozwa na Paul Muite kwamba masuala yaliyotolewa katika maombi hayo sita yalikuwa mazito ya kikatiba.

"Kwa kuzingatia maslahi makubwa ya umma suala hili limeibua na kuwa la kwanza la aina yake nchini Kenya ambapo Naibu Rais wa Jamhuri anaondolewa kwa mchakato wa kushtakiwa, ni maoni yangu kwamba suala hili linastahili michango ya Bunge ili kujitangaza kwenye mchakato unaofuata katiba ili kutumika kama vigezo vya shughuli za baadaye za aina hii," Jaji Mugambi aliamua.

Baada ya Bunge kupiga kura ya kutaka aondolewe madarakani, Gachagua sasa anafaa kufika mbele ya Bunge la Seneti kujitetea, na hapo baadaye maseneta pia watapiga kura.

Bunge la Seneti nchini Kenya limeamua kusikiliza hoja ya kumtimua Naibu Rais Rigathi Gachagua katika kikao cha mashauriano kitakachofanyika Oktoba 16 na 17, 2024.

Hata hivyo, Mahakama itatoa uamuzi Jumanne asubuhi ikiwa itazuia Seneti kuzingatia azimio la Bunge la Kitaifa la kumshtaki Gachugua.

TRT Afrika