Bodi ya Utendaji ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) imeidhinisha Somalia kupata usaidizi zaidi wa kifedha.
“Somalia itapewa takriban dola za kimarekani milioni 9.4 kwa ajili ya kusaidia utekelezaji wa mipango wa maendeleo wa kitaifa," IMF imesema katika taarifa.
Fedha hizi zitatolewa chini ya mpango wa IMF wa usaidizi wa kifedha wa muda kwa nchi za kipato cha chini zenye madeni ya muda mrefu na matatizo ya malipo.
Bodi ya shirika la IMF imeridhika na jitihada za maendeleo na mabadiliko nchini Somalia baada ya kufanya awamu ya tano ya uangalizi wa ufadhili wa mikopo kwa Somalia.
“Licha ya changamoto kubwa, ikiwa ni pamoja na kuendelea kwa mzozo mkali wa chakula, Somalia imedumisha kasi kubwa ya mageuzi na utendaji wa programu za kuijiendeleza,” shirika la IMF limesema.
Mkopo huu mpya unaleta jumla ya malipo ya Somalia chini ya mpango uliopanuliwa wa mikopo na mfuko wa upanuzi wa hazina chini ya IMF hadi dola milioni 386.1 za Marekani.