Tume ya Pamoja ya Ufuatiliaji na Tathmini ya Sudan Kusini, yaani, Reconstituted Joint Monitoring and Evaluation Commission (RJMEC) imesema Sudan Kusini haionokeni kuwa tayari kwa uchaguzi wake mkuu uliopangwa kufanyika mwezi Disemba 2024.
"Takriban miezi saba kabla ya uchaguzi, bado hakuna ishara wa maandalizi ya kutosha kwa ajili ya uendeshaji wa uchaguzi na utekelezaji wa majukumu muhimu yanayohusiana na uchaguzi, " Mwenyekiti wa Muda wa RJMEC, balozi Meja Jenerali Charles Tai Gituai amesema katika taarifa.
Iwapo uchaguzi huu utafanyika, basi hii itakuwa mara ya kwanza kwa Sudan Kusini kufanya uchaguzi tangu ipate uhuru mwaka 2011.
Katika tathmini yake ya Mkataba Uliohuishwa wa Amani nchini Sudan Kusini balozi Gituai alisema majukumu haya muhimu, miongoni mwa mengine, ni pamoja na utendakazi kamili na ufadhili wa Baraza la Vyama vya Siasa.
Tathmini hiyo pia imeonyesha kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi haionekani kuwa tayari pamoja na Tume ya Taifa ya Marekebisho ya Katiba. Bado kutengeneza katiba ya kudumu itakayoongoza uendeshaji wa uchaguzi haujafanyika.
Aidha, alisema, mwenendo wa Tume inayohusiana na uchaguzi kama vile uanzishaji wa vyombo vya usimamizi wa uchaguzi katika ngazi ya jimbo, uwekaji wa taratibu za daftari la wapiga kura na uandikishaji, na kusaidia elimu ya uraia na uhamasishaji wa wapiga kura, uchapishaji wa daftari la wapiga kura miezi sita kabla ya kufanyika kwa uchaguzi, pia unasubiriwa.
Aidha alieleza kuwa kazi nyengine zinazosubiri kukamilika ni pamoja na mchakato wa marekebisho ya mahakama, mapitio ya Sheria ya Mahakama na uanzishwaji wa Mahakama ya Katiba na kutunga Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Usalama wa Taifa ya mwaka 2023 ili pamoja na mambo mengine kuunda nafasi ya kiraia na kisiasa kwa ushiriki wa wananchi katika utawala.
Amesema ni muhimu kwamba mazungumzo kati ya vyama yaharakishwe ili kutoa ufafanuzi wa njia ya kusonga mbele.
"Hii ingesaidia watu wa Sudan Kusini kujiandaa vya kutosha na kuwezesha uhamasishaji wa rasilimali kwa wakati na jumuiya ya kikanda na kimataifa kusaidia mchakato," alisema.
Zaidi ya hayo, balozi Gituai aliibua wasiwasi juu ya kuendelea kwa ghasia kati ya jumuiya katika maeneo mbalimbali ya nchi, kama vile Tambura, Twic, na sehemu za mkoa wa Abyei.
"Hii inasisitiza umuhimu wa kuunganishwa kikamilifu kwa vikosi vyote na kutumwa tena ili kutoa usalama katika maeneo yote ya nchi," Gituai aliongezea.
Rais Salva Kiir ametangaza kuwa atagombea kiti katika uchaguzi huo huku naibu wake ambaye pia ni mpinzani wake wa kisiasa, Riek Machar tayari amelalamika kuwa nchi haipo tayari kwa uchaguzi.