Tangu Aprili 2023 mapigano yanaendelea kati ya Jeshi la Sudan na Vikosi vya RSF. /Picha: X@AbiyAhmedAli

Na Coletta Wanjohi

Addis Ababa, Ethiopia

Kabla ya Mkutano wa Umoja wa Afrika wa 2025 jijini Addis Ababa, Ethiopia, shirika la kikanda la IGAD na Umoja wa Mataifa wamefanya mkutano wa ngazi ya juu kujadilli madhila wanayopitia watu Sudan.

Sudan ni mwanachama wa shirika hilo la kikanda.

"Mgogoro huu si wa Sudan pekee ni suala la kikanda na kimataifa," alisema Abiy Ahmed Waziri Mkuu wa Ethiopia kwenye kikao kilichofanyika katika Shirika la Uchumi kwa Afrika la Umoja wa Mataifa mjini Addis Ababa.

Tangu Aprili 2023 mapigano yanaendelea kati ya Jeshi la Sudan na Vikosi vya RSF.

Rais wa Kenya William Ruto anasema mzozo huo umeharibu taifa ambalo miaka minne tu iliyopita lilikuwa katika muelekeo wa kupata utulivu na kupiga hatua kimaendeleo.

"Maendeleo ya Sudan ya kujitosheleza kwa chakula yalionekana walipopata mavuno mazuri ya ngano na kilimo cha miwa, yote haya yamebadilishwa na vita huku zaidi ya nusu ya wakazi wa Sudan wakiwa hawana chakula kwa sasa," Rais Ruto ameuambia mkutano wa Addis Ababa.

Ethiopia inaahidi mchango wa dola milioni 15 katika kushirikiana katika suala la Sudan. /Picha: @AbiyAhmedAli

Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa utazindua mpango wa misaada kwa watu wa Sudan na pamoja na mradi wa kuwasaidia wakimbizi wa Sudan.

"Mipango yote haya kwa pamoja, yanahitaji dola bilioni 6, kusaidia karibu watu milioni 21 ndani ya Sudan na wengine karibu milioni 5 hasa wakimbizi katika nchi jirani, matatizo makubwa kwa watu, ambayo hayajawahi kutokea katika bara la Afrika," Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Gutteres amesema.

Ethiopia ambayo ina mpaka na Sudan na inabeba mzigo mkubwa wa mapigano hayo hii ni kupitia idadi kubwa ya wakimbizi kutoka nchini humo wanaoingia Ethiopia. Nchi hiyo imeahidi kutoa fedha.

"Ethiopia inaahidi mchango wa dola milioni 15 katika kushirikiana kuhusu suala la Sudan," Abiy Ahmed ameahidi.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Gutteres anasema "Sudan iko katika mzozo wa kiwango cha hatari na cha ukatili. Mgogoro ambao unazidi kuenea katika maeneo mengine.

Viongozi wa Afrika wanasema mzozo huu wa kisiasa na tatizo kubwa kwa watu wa nchini Sudan unahitaji kufanyiwa tathmini ya haraka na Umoja wa Afrika pamoja na Jumuiya ya kimataifa.

"Tunajua watu wa Sudan wanataka nini. Tumefanya mashauriano ya kina na raia wa Sudan na wanataka kusitishwa kwa mapigano mara moja na raia wawe na usalama," Gutteres ameongeza.

Katika mkutano wa ahadi za misaada uliofanyika Paris, Ufaransa kwa ajili ya Sudan mwezi Aprili 2024, Kenya iliahidi dola milioni 1. na katika mkutano huu wa 2025 imeongeza dola milioni 1 zaidi, yote haya ni katika juhudi za kuwasaidia watu wa Sudan.

TRT Afrika