Polisi wanawasaka washukiwa saba akiwemo dereva wa Lori aliyesababisha mlipuko, ambaye haijulikani iwapo aliponea au alifariki katika mlipuko. /Picha : Kenya Red Cross

Idadi ya waliofariki kutokana na mlipuko wa gesi katika eneo la makazi jijini Nairobi imefikia sita huku mamia wengine wengi wakiendelea kupokea matibabu ya majeraha mabaya.

Duru za serikali zinasema kuwa majeruhi wamelazwa katika hospitali mbalimbali ikiwemo wengine 20 waliopelekwa hoispitali ya rufaa ya Kenyatta kutokana na uhatari wa majeraha yao.

"Tunasikitika kuripoti kwamba watu watatu zaidi wamefariki kutokana na majeraha yao na hivyo kuongeza idadi ya waliofariki kutokana na tukio la Moto Embakasi hadi sita," alisema Msemaji wa Serikali Isaac Mwaura katika taarifa iliyotolewa Jumatatu.

Wakati huo huo, serikali imemkamata mshukiwa mmoja kufuatia ajali hiyo ya mlipuko wa gesi iliyosababisha vifo vya watu 6 na kuwajeruhi wengine zaidi ya 300.

Hii inafuatia agizo la Rais William Ruto la kukamatwa na kufunguliwa mashtaka kwa maafisa waliotoa leseni kwa kiwanda hicho cha gesi kufanya kazi.

Kamanda wa Polisi wa Nairobi Adamson Bungei amethibitisha kukamatwa kwa mshukiwa na kusisitiza ahadi ya kuwakamata watu wote waliohusika.

''Tuna mmoja wa maafisa chini ya ulinzi na msako wa kuwatafuta zaidi ikiwa ni pamoja na wamiliki wa mtambo huu unaendelea," alisema Bungei.

Taarifa ya polisi inasema kuwa washukiwa wengine saba wanatafutwa kuhusiana na kesi hiyo akiwemo, mmiliki wa mtambo huo wa kujaza gesi haramu, na mshirika wake, pamoja na dereva wa lori anayeshukiwa kusababisha mlipuko huo. Hali ya dereva, iwe alitoroka au aliangamia katika tukio hilo, bado haijathibitishwa.

Kama sehemu ya uchunguzi unaoendelea kuhusu mlipuko huo na vifo vilivyotokana na mlipuko huo, mamlaka inapanga kufanya uchunguzi wa miili ya wahasiriwa, na wale watakaopatikana na hatia wanaweza kukabiliwa na mashtaka yanayohusiana na mauaji.

Waathiriwa na familia zao wanatarajia kulipwa fidia kutoka kwa wamiliki wa yadi ambapo mlipuko ulitokea na kutoka kwa serikali pia.

TRT Afrika