Idadi ya waliofariki katika mlipuko wa kiwanda cha gesi nchini Kenya imeongezeka hadi kufikia watu saba baada ya mmoja kufariki kutokana na majeraha, msemaji wa serikali Isaac Mwaura amesema.
Alhamisi tarehe 1 Februari 2024, mwendo wa saa tano na nusu usiku, kulitokea mlipuko mkubwa katika eneo la Embakasi, Kaunti ya Nairobi.
Takribani watu 280 walijeruhiwa wakati lori lililokuwa limebeba mitungi ya gesi kulipuka.
"Katika harakati zetu za kutafuta haki kwa waathirika watu wanne walifikishwa katika mahakama ya Milimani na kushtakiwa kwa mauaji," Dk. Isaac Mwaura msemaji wa serikali amesema katika taarifa.
Mahakama inafaa kutoa uamuzi wa maombi ya washukiwa leo tarehe 7.
"Katika jitihada nyengine, waathiriwa wote ambao walikuwa wamewekwa katika ukumbi wa jamii wa Embakasi wamerudishwa nyumbani au kupewa makazi mapya. Serikali inaendelea kutoa usaidizi zaidi wa chakula na mahitaji mengine kuwasaidia kurejea katika maisha yao ya kawaida," Mwaura ameongezea.
Taasisi ya Petroli ya Afrika Mashariki ilisema mlipuko huo ulitokea kwenye "eneo ambalo sio rasmi kujaza na kuhifadhi gesi," ambalo mmiliki wake na baadhi ya wateja walitiwa hatiani na kuhukumiwa Mei 2023.
Taarifa hiyo pia imesema, kuwa mmiliki aliendelea kuendesha kituo "bila hata viwango vya chini vya usalama na wafanyakazi waliohitimu wa LPG kama inavyotakiwa na sheria."
Maafisa kutoka Shirika la Kitaifa la Kusimamia Mazingira (NEMA) wameshtakiwa kwa kutoa leseni kimakosa kwa kiwanda cha kujaza na kuhifadhi gesi ya LPG katika eneo hilo lenye watu wengi.