Maandamno yaliyoanza siku ya Jumanne 25 Juni, kufuatia kupitishwa kwa mswada tata na Bunge la Taifa nchini Kenya, yametatiza hali ya utulivu, usafiri na biashara katika baadhi ya miji haswa Nairobi.
Ingawaje hali ya utulivu imeanza kushuhudiwa baada ya Rais wa nchi hio, William Ruto kuukataa mswada huo na kuurudisha bungeni.
Kulingana na vyombo vya habari nchini Kenya, maduka ambayo yalikuwa yamefungwa hapo mbeleni kwa sababu ya maandamano yamefunguliwa na biashara kurudi kama kawaida. Wachuuzi na wafanyabiashara pia wamerejea mjini.
Usafiri pia umerudi kwa hali yake ya kawaida, huku wakaazi wakionekana kuendelea na shughuli zao za kila siku bila hofu iliyokuwa imekumba jiji hilo katika siku chache zilizopita.
Baadhi ya wamiliki walionekana wakijaribu kusafisha maeneo yao ya kazi kwa ajili ya kuanza upya.
"Maandamano haya yalituathiri sana, wakati wa maandamano baadhi ya waandamanaji walitumia fursa hiyo kuiba na kuharibu mali ya watu, tunafurahi kuona mambo yanarejea katika hali ya kawaida," alisema mmoja wa wafanyabiashara katika jiji la Nairobi.
Hali kadhalika, idadi ya polisi pia imeonekana kupungua, ikilinganishwa na idadi ya hapo awali walipopelekwa kudumisha amani.