Licha ya kusitishwa mapigano kupatikana kwa huduma muhimu kama za matibabu imekuwa ngumu kupatikana. /Picha: Reuters

Hospitali katika mji mkubwa wa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Goma, zinatatizika kutibu mamia ya wagonjwa waliojeruhiwa, huku baadhi wakiripoti uhaba wa dawa siku chache baada ya kundi la waasi la M23 kutangaza kusitisha mapigano.

Stephan Goetghebuer, meneja miradi katika shirika la usaidizi la Madaktari Wasio na Mipaka (MSF), aliiambia Anadolu katika mahojiano Jumatano kwamba jiji lilikuwa shwari, lakini hali katika hospitali bado ni mbaya.

Ghasia huko Goma, mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini, zilizuka wiki mbili zilizopita wakati M23 ilipoanzisha mashambulizi makubwa dhidi ya vikosi vya serikali.

Shirika la Afya Duniani (WHO) limeripoti kuwa zaidi ya watu 900 wameuawa katika kipindi hicho, na karibu 3,000 kujeruhiwa.

Maelfu wameyakimbia makazi yao, wengi wao wakikimbilia nchi jirani ya Rwanda, wakiwemo wafanyakazi kutoka mashirika ya kimataifa kama vile UN na Benki ya Dunia. Kundi la M23 lilitangaza kusitisha mapigano Jumatatu baada ya wiki mbili za mapambano na jeshi la DRC kwa ajili ya kudhibiti mji wa Goma.

Hali mbaya kwa watu

Goetghebuer alisema huduma za upatikanajai wa maji zimerejea katika baadhi ya maeneo mjini humo ambako kunaishi takriban watu milioni tatu, huku kukiwa na uhaba wa dawa hospitalini na njia za usafiri hadi Goma bado hazijafunguliwa.

“Hospitali za Goma zimepokea mamia ya wagonjwa waliojeruhiwa,’’ alisema, akiongeza kuwa hospitali mbili ambazo vyumba vyake vya upasuaji vinasaidiwa na Shirika la MSF zinafanya kazi muda wote wa kuhudumia wagonjwa.

"Hali kwa watu ni mbaya sana," amesema kwa kupitia njia ya simu.

Goetghebuer alisema bado kuna baadhi ya wagonjwa wapya waliojeruhiwa ambao wanakuja hospitali kutafuta matibabu.

Amesema walikuwa wamejificha na kuogopa kutoka, lakini kuna hali ya kawaida katika jiji hilo na wanakuja kutafuta matibabu.

"Pia kuna suala la waliokimbia makazi yao. Kulikuwa na maelfu ya watu ambao walikuwa wakiishi katika kambi za muda huko Goma kutokana na mapigano ya hivi majuzi. Baadhi ya kambi hizo zimeharibiwa. Baadhi ya watu hao wamefukuzwa,’’ na kuongeza kusema kuwa wengine wanaishi mafichoni.

Mazungumzo ya kutafuta suluhu

Taarifa iliyotolewa na Rais wa Kenya William Ruto, wawili hao watakutana katika mkutano wa pamoja wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), baada ya Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania kuridhia nchi yake kuwa mwenyeji wa mkutano huo.

Hatua hiyo inafuatia makubaliano kati ya mwenyekiti wa SADC Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe na Rais William Ruto wa Kenya, ambaye pia ni mwenyekiti wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya EAC.

“Rais Samia Suluhu Hassan amekubali kuwa mwenyeji wa mkutano huo ambao unalenga kutafuta suluhu ya mgogoro wa Mashariki mwa DRC," alisema Rais Ruto.

Kulingana na Rais Ruto, wawili hao wamethibitisha uwepo wao kwenye mkutano huo wa pamoja ambao utatanguliwa na mkutano wa mawaziri siku ya Ijumaa, kabla ya Wakuu wa EAC na SADC hawajakutana siku ya Februari 8, 2025.

Rais Ruto pia amesema kuwa amewashirikisha jambo hilo Marais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini, Yoweri Museveni wa Uganda na Hassan Sheikh Mohamud wa Somalia.

AA