Waziri Mkuu mpya wa Haiti Alix Didier Fils-Aime aliahidi kuweka nguvu, ujuzi na uzalendo katika huduma ya kazi ya kitaifa/ Photo:  Reuters

Baraza la Urais wa Mpito nchini Haiti lilimteua mfanyabiashara na aliyekuwa seneta Alix Didier Fils-Aime kuwa Waziri Mkuu mpya wa nchi hiyo baada ya kumfuta kazi Garry Conille.

Conille, ambaye aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu mwezi Mei, amewahi kufanya kazi kama afisa wa Umoja wa Mataifa.

Serikali yake ilipewa jukumu la kupanga njia ya uchaguzi ujao wa urais. Hata hivyo, alifukuzwa kazi baada mzozo wa mamlaka ya kisiasa na baraza hilo kuhusu mamlaka wa serikali.

Baada ya kujua kuhusu mpango wa kumfuta kazi, alisema hatua hiyo ni kinyume cha katiba.

Waziri Mkuu mpya amesema yuko tayari kwa kazi na changamoto zake.

"Tuna awamu ya mpito yenye kazi nyingi ya kufanya: kazi ya kwanza muhimu, ambayo ni sharti la mafanikio, ni usalama," Fils-Aime alisema katika hotuba yake ya kwanza.

Alisema anafahamu "hali ngumu" ya Haiti lakini aliahidi kuweka "nguvu zangu, ujuzi wangu na uzalendo katika huduma ya kazi ya kitaifa."

Mgogoro wa usalama

Baraza la urais lenye wajumbe tisa ambalo liliundwa mwezi Aprili, lilichukua hatamu ya uongozi wa nchi hiyo baada ya kujiuzulu kwa Waziri Mkuu wa awali, Ariel Henry, kutokana na mzozo wa kiusalama ambao umekuwa ukiendelea kwa miaka mingi.

Rais wa mwisho wa Haiti, Jovenel Moise, aliuawa Julai 2021, na hakuna uchaguzi ambao umefanyika tangu wakati huo.

Henry alilazimishwa kuondoka katika wadhifa wake na magenge ambayo yamepata udhibiti wa sehemu kubwa ya mji mkuu, Port-au-Prince, na kuwalazimisha mamia ya maelfu ya wakazi kutoka katika nyumba zao.

Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Haiti ulifungwa Jumatatu baada ya magenge kufyatulia risasi ndege ya Shirika la Ndege la Spirit Airlines iliyokuwa ikitua Port-Au-Prince, Shirika hilo la ndege lilisema.

Usalama ulioimarishwa

Kufuatia tukio hilo, ndege hiyo ilielekezwa Jamhuri ya Dominika. Kulingana na ripoti za awali, risasi ilimpiga mmoja wa wafanyakazi.

Licha ya kuwepo kwa Ujumbe wa Kimataifa wa Usaidizi wa Usalama wa Kimataifa unaoongozwa na Kenya unaoungwa mkono na Umoja wa Mataifa, nchi hiyo inaendelea kuona ongezeko la mauaji, utekaji nyara, njaa, na maeneo yanayodhibitiwa na magenge.

Umoja wa Mataifa umeripoti kuwa takriban watu 4,900 wameuawa nchini Haiti kati ya Januari na Septemba mwaka huu, na watu wapatao 700,000 wamekimbia makazi yao ndani ya ardhi ya Haiti.

TRT Afrika