Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji nchini Tanzania (EWURA) imetangaza kushika kwa bei za bidhaa ya mafuta ya petrol kuanzia Disemba 4, 2024.
Katika taarifa yake kwa umma, EWURA imeainisha bei ya lita moja ya petrol kuwa ni Dola Za Kimarekani 1.10 (Shilingi za Kitanzania 2,898), huku mafuta ya dizeli yakinunuliwa kwa Dola 1.06 (Shilingi za Kitanzania 2,779) kwa lita.
“Gharama za uagizaji mafuta zimeongezeka kwa wastani wa asilimia 7.26 kwa petroli na kupunguza kwa asilimia 12.80 ka dizeli na wastani wa asilimia 7.10 kwa mafuta ya taa katika bandari ya dar es Salaam,” ilisema taarifa hiyo.
EWURA imeongeza kuwa kwa mwezi Disemba 2024, bei za kikomo za mafuta zimekokotolewa kwa kuzingatia bei za soko la Uarabuni za mwezi Novemba 2024.
Ikilinganishwa na Mwezi Oktoba 2024, bei za mwezi Novemba zimepungua kwa asilimia 0.29 kwa mafuta ya petroli; kuongezeka kwa asilimia 2.11 kwa mafuta ya dizeli na asilimia 2.28 kwa mafuta ya taa.
“Kampuni za mafuta ziko huru kuuza bidhaa za mafuta ya petroli kwa bei ya ushindani isipokuwa bei hizo zisizidi bei kikomo au kuwa chini ya bei iliyoruhusiwa kama zilivyokokotolewa kwa mujibu wa Kanuni za EWURA za Kupanga Bei za Mafuta,” iliongeza taarifa hiyo.
Hali kadhalika, mamlaka imevitaka vituo vyote vya mafuta kuchapisha bei za bidhaa za mafuta katika mabango yanayoonekana bayana yakionesha bei za mafuta, punguzo, vivutio vya kibiashara vinavyotolewa na kituo husika.