Hii ni mara ya tatu kwa bunge hilo kumtimua Gavana Mwangaza, kufuatia majaribio mawili ya awali yaliyositishwa na Mahakama Kuu ya Meru.
Katika hoja ya kumtimua, Kinya alimshutumu Mwangaza kwa makosa makuu matatu yakiwemo ukiukaji mkubwa wa Katiba ya Kenya, ukiukaji wa sheria za kitaifa na kaunti, na matumizi mabaya ya ofisi.
Kinya aliendelea kumshutumu na kudai kuwa Mwangaza alitenda utovu wa nidhamu kwa kupotosha umma kuhusu pesa zilizochangishwa kwa ajili ya familia ya mwanablogu aliyeuawa Daniel Muthiani almaarufu Sniper.
Alidai kuwa gavana huyo wa kaunti alisema uwongo kwamba Sh86 milioni zilikusanywa kupitia nambari ya Paybill, huku Sh286,516 pekee zilikusanywa.
Muthiani, mwanablogu maarufu, alitekwa nyara huko Meru, na mwili wake kupatikana katika eneo jirani la Tharaka Nithi mnamo Desemba mwaka jana, na hivyo kuzua mvutano wa kisiasa.
Spika wa Bunge Ayub Bundi alisema, "Aliamua kwamba hoja ya kumtimua ilikuwa kisheria mbele ya bunge licha ya kuwa kuna kesi iliyowasilishwa mahakamani. Alisema kuwa Gavana huyo alialikwa kujitetea lakini hakujibu. "Mheshimiwa bado hajajibu mwaliko huo."
Mwangaza atasubiri uamuzi wa Seneti kufahamu iwapo bunge hilo litamwokoa au kumfurusha. Mwangaza anakuwa gavana wa kwanza kushtakiwa mara kadhaa nchini.