Umoja wa Afrika ulichukua rasmi kiti chake kama mwanachama mpya wa G20 Jumamosi kwa mwaliko wa Waziri Mkuu wa India Narendra Modi.
Kupanuka kwa muungano huo ni ushindi wa kidiplomasia kwa Modi, ambaye anakabiliwa na uchaguzi wa kitaifa mwaka ujao na ametumia haki za kuandaa kongamano la mwaka huu kupiga msasa sifa yake kama mwanasiasa wa kimataifa.
Kabla ya hotuba yake ya ufunguzi, Modi alimsalimia mwenyekiti wa Umoja wa Afrika na Rais wa Comoro Azali Assoumani kwa kumbatio la udugu.
"India ilitoa pendekezo la kutoa uanachama wa kudumu wa G20 kwa Umoja wa Afrika. Ninaamini kuwa ni jambo ambali tumekubaliana sote," Modi alisema katika hotuba yake ya ufunguzi wa mkutano huo.
"Kwa idhini ya kila mtu, namwomba mkuu wa Umoja wa Afrika kuchukua kiti chake kama mwanachama wa kudumu wa G20," aliongeza, akigonga chali ya sherehe.
Assoumani kisha akaketi kati ya viongozi wa dunia kwa mapokezi ya waziri wa maswala ya kigeni wa India S. Jaishankar.
Kupata mwafaka kati ya wanachama kumezidi kuwa vigumu katika miaka ya hivi karibuni na mgawanyiko mkubwa juu ya vita vya Ukraine, shirika la habari la AFP linaripoti.
"Ulimwengu una shida kubwa ya uaminifu," Modi alisema katika hotuba yake ya ufunguzi.
"Vita imefanya upungufu huu wa uaminifu kuwa mkubwa zaidi. Ikiwa tunaweza kushinda Covid, tunaweza pia kushinda migogoro hii na kutoaminiana."
Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa alieleza kufurahishwa na nchi yake kwa kuandikishwa kwa Umoja wa Afrika.