Ni siku chache tu kabla ya Afrika Mashariki kuchukua uongozi wa tume ya Umoja wa Afrika.
Raila Odinga wa Kenya, Mahamoud Ali Youssouf wa Djibouti na Richard Randriamandrato wa Madagascar wanawania nafasi ya uenyekiti wa tume ya hiyo.
Uchaguzi utafanywa na marais na viongozi wa serikali watakapokutana kwa mkutano wao wa kila mwaka jijini Addis Ababa nchini Ethiopia tarehe 15 na 16 Februari.
Mwenyekiti wa tume ya AU atahudumu kwa miaka minne na anaweza kuongeza muhula mwingine mmoja, iwapo atachaguliwa tena.Kwa kupitia kura ya siri marais watamchagua Mwenyekiti na naibu wake.
Kwa kawaida kuna jumla ya kura 55 ikiashiria nchi wanachama wa Umoja wa Afrika. Lakini mwaka huu nchi sita hazitapiga kura – nazo ni Mali, Guinea, Burkina Faso, Gabon, Niger na Sudan ambazo uanachama wao wa AU umesitishwa kwa muda kutokana na mataifa hayo kuwa na mamlaka ya kijeshi.
Hivyo mshindi wa uenyekiti wa tume ya AU lazima apate theluthi mbili ya kura 49 ambayo ni kura zisizopungua 32.Mchakato wa kupiga kura huanza na wagombea wote kuwepo kwenye mpambano.
Upigaji kura unafanyika mara tatu na iwapo hakuna atakayepata theluthi mbili ya kura baada ya hatua ya tatu, hatua inayofuata itakuwa na wagombea wawili (2) waliopata kura nyingi zaidi na mgombea aliye na kura chache ataondolewa.
Iwapo mgombea aliyebakia atashindwa kupata theluthi mbili ya kura inayohitajika katika awamu hiyo, Mwenyekiti anatakiwa kusitisha uchaguzi kwa muda.
Hapa tunazunguma Mwenyekiti ambaye ni rais wa nchi ambayo iko kwenye uongozi wa mwaka husika wa AU.
Kila mwaka mataifa hupokezana jukumu la Uenyekit, na mwaka huu ni zamu ya Visiwa vya Comoro.
Mwenyekiti akisimamisha uchaguzi kwa mgombea kukosa theluthi mbili ya kura, marais wataamua kuhusu lini uchaguzi huo utarudiwa.
Iwapo uchaguzi wa Mwenyekiti utasimamishwa, Naibu Mwenyekiti wa Tume atakaimu wadhifa huo/ Je, ni Kenya, Djibouti au Madagascar itakayopata Mwenyekiti wa tume ya Umoja wa Afrika?