Bunge la Ethiopia limepitisha sheria ya kuruhusu benki za kigeni kuingia katika sekta ya fedha ya nchi hiyo na kuwekeza.
Sheria inaziruhusu benki za kigeni kuanzisha kampuni, kufungua matawi au ofisi za uwakilishi.
Hata hivyo, kuna masharti kwa benki za kigeni zinazotaka kuungana na benki za ndani.
Benki za kigeni zinaruhusiwa kupata hisa katika benki za Ethiopia, kwa umiliki wa asilimia 40 kwa wawekezaji wa kimkakati wa kigeni na kuruhusu nyongeza ya asilimia 7 hadi 10 kwa wawekezaji wa kigeni wasio wa kimkakati.
Sheria pia inaweka ukomo wa umiliki wa pamoja wa raia wa kigeni na mashirika ya Ethiopia yanayomilikiwa na wageni hadi asilimia 49, kuhakikisha umiliki mkubwa unabaki kuwa wa Ethiopia.
Uidhinishaji huo wa wabunge umekuja miezi sita baada ya Baraza la Mawaziri kupitisha rasimu ya kuboresha biashara ya sekta ya benki ambayo baadaye ilitumwa kwa baraza kwa ajili ya kuidhinishwa.
Mnamo Juni 2023, serikali ilitangaza nia yake ya kutoa hadi leseni tano za benki kwa wawekezaji wa kigeni katika kipindi cha miaka mitano kama sehemu ya mkakati wa kufungua sekta ya huduma za kifedha kwa ushindani wa kigeni.
Licha ya uhuru huo, baadhi ya wabunge walionyesha wasiwasi wao juu ya athari kwa benki za ndani huku wengine wakihofia ikiwa benki binafsi zitastahimili ushindani wa kigeni.
Mamo Mihretu, Gavana wa Benki ya Taifa ya Ethiopia, aliwahakikishia wabunge kwamba ingawa baadhi ya benki zinakabiliwa na changamoto matatizo hayo yote yanashughulikiwa na udhibiti wa Benki Kuu.
Benki 32 zinafanya kazi nchini Ethiopia, huku Benki ya Biashara ya Ethiopia inayomilikiwa na serikali ikishikilia 21.5% ya jumla ya mtaji wa benki.