Ethiopia itachelewesha awamu ijayo ya kujaza bwawa jipya la kuzalisha umeme kwenye Mto Nile.
Kujazwa kwa Bwawa la Grand Ethiopian Renaissance (GERD) kutaahirishwa hadi Septemba, Waziri Mkuu Abiy Ahmed alisema Ijumaa wakati wa kikao katika baraza la wawakilishi la Ethiopia.
Ikikamilika bwawa hilo lina uwezo wa kuzalisha megawati 6000 ya umeme.
Hapo awali, awamu ya nne ya kufungulia maji ya mto Nile kuingia katika bwawa hili kulikuwa kumepangwa mapema Agosti.
Abiy alisisitiza kujitolea kwa Ethiopia kushughulikia wasiwasi wa mataifa ya chini ya mto huo, ikiwa ni pamoja na Sudan Kusini, Sudan na Misri, kuhusu mchakato wa kujaza bwawa hilo.
"Ujazaji wa mwaka huu utafanyika tofauti na awamu tatu zilizopita , ikiwa maji yatafunguliwa kuingia kwa bwawa kwa njia ya kupunguza wasiwasi wa nchi jirani," waziri mkuu alisema. "Badala ya kukamilisha kujaza mapema Agosti kama katika raundi zilizopita, itafanywa mwanzoni mwa Septemba au mwishoni mwa Agosti."
Mvutano wa kidiplomasia
Katika jitihada za kudumisha uhusiano mzuri na majirani zake, Abiy alithibitisha kwamba Ethiopia inaelewa wasiwasi wa mataifa ya chini ya mto na ilikuwa na nia ya kuyazingatia wakati wa kujaza GERD.
Bwawa hilo ni mradi mkuu wa kuzalisha umeme kwa maji kwenye Mto wa Blue Nile, lakini limekuwa chanzo cha mvutano wa kidiplomasia kati ya Ethiopia, Sudan na Misri.
Sudan na Misri zimetoa wasiwasi kuhusu athari zinazoweza kusababishwa na bwawa hilo katika usambazaji wa maji na shughuli za kilimo.
Kwa kuongeza muda wa kujaza, Ethiopia inasema inalenga kuhakikisha kwamba masuala haya yanashughulikiwa kupitia mazungumzo na mashauriano.
GERD, ikishafanya kazi kikamilifu, inatarajiwa kuzalisha kiasi kikubwa cha umeme kwa Ethiopia, kusaidia juhudi za maendeleo ya nchi hiyo na kutoa ufikiaji wa nishati kwa mamilioni ya raia wake.