Wazo la Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed,  la kukuza ngano Inayostahimili mazingira tofauti   liliungwa mkono na ufadhili wa dola milioni 94 hasa kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika / picha kutoka Abiy Ahmed kwa X 

Na Coletta Wanjohi

Istanbul, Uturuki

Kuanzia mijini hadi vijiji vya Ethiopia mkate ni sehemu muhimu ya kila mlo.

Uokaji unaotumia njia ya kitamaduni huwezesha kupata mkate safi licha ya umbali ambao mtu anasafiri katika nchi.

"Nchini Ethiopia kila mtu anajua kuoka mkate, katika mazingira ya kisasa au ya kitamaduni, mkate ni muhimu sana kwetu," Beza Meseret anaiambia TRT Afrika.

Katika miji maduka ya mikate ya kawaida huwauzia watu bidhaa zilizookwa kwa matumizi ya kila siku na sherehe.

Hawa wote wanahitaji ngano nyingi, ambayo nchi ilikuwa inaagiza kwa wingi kutoka nje.

"Kihistoria, Ethiopia ilitumia takriban dola bilioni 1 kila mwaka kwa uagizaji wa ngano ili kukidhi mahitaji ya ndani, kwani uzalishaji wa ndani haukuwa wa kutosha," ofisi ya Waziri Mkuu wa Ethiopia imesema katika ripoti iliyoitoa kwa TRT Afrika.

Kupanda aina ya ngano iliyoimarishwa kulimaanisha uvunaji ulifanyika mara mbili, sehemu fulani ya ardhi ilifanyiwa umwagiliaji wa maji huku nyingine ikiachwa ili kupitia msimu wa asili wa uzalishaji wa ngano/ Picha: Ofisi Waziri Mkuu Ethiopia  

Hata hivyo, Waziri Mkuu wa nchi hiyo Abiy Ahmed alianza mradi kabambe wa kuongeza uzalishaji wa ngano wa ndani, ambayo aliuambia Mkutano wa Umoja wa Afrika wa 2025, kwamba umekuwa na mafanikio makubwa.

"Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, tumeongeza maradufu ardhi yetu inayolimwa, na kuongeza uzalishaji wa mazao hadi karibu tani milioni 70 huku ngano ikichukua asilimia 40 ya kwa ujumla," Waziri Mkuu Ahmed aliuambia mkutano wa AU mjini Addis Ababa, 15 Februari 2025.

Wazo la Waziri Mkuu la kukuza ngano Inayostahimili mazingira yote ya hali ya hewa (CREW) liliungwa mkono na ufadhili wa dola milioni 94 hasa kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika.

Hili lilifanywa chini ya mpango wa benki ya 'Technologies for African Agricultural Transformation' (TAAT) ambao lengo lake ni kusaidia Afrika kukuza uzalishaji wake wa kilimo kwa kutumia teknolojia zenye matokeo mazuri.

Nchi 27 ziliratibiwa kuijunga na mradi huu.

Kenya, Zambia, Zimbabwe, Nigeria na Ethiopia zilitambuliwa kwa uzalishaji wa ngano.

"Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, Mkataba wa Ngano wa TAAT umeshirikiana na serikali ya Ethiopia na makampuni ya mbegu kufanya aina za ngano zinazostahimili joto zipatikane kwa wakulima katika nyanda za chini za nchi, ambapo joto la juu la mchana hupunguza mavuno kutoka kwa aina za ngano za kawaida," AfDB imesema katika taarifa yake kwa vyombo vya habari.

Mikoa ya Afar, Amhara, Oromia, na Somalia ya Ethiopia ndiyo eneo linalolengwa la uzalishaji.

Takwimu kutoka wizara ya kilimo ya Ethiopia zinaonesha kuwa takriban wakulima milioni 3.4 walihusika katika uzalishaji wa ngano ya umwagiliaji mwaka 2023/24 / picha: Ofisi ya Waziri Mkuu wa Ethiopia 

AfDB ilisema mradi huo kwa ujumla "utawanufaisha watu milioni 2.3, asilimia 50 kati yao wanawake, kwa kuongeza mapato ya kaya, kuunda nafasi za kazi na ujasiriamali, na kuimarisha upatikanaji wa chakula na lishe."

Safari ya kujitosheleza kwa ngano

Ofisi ya Waziri Mkuu wa Ethiopia imeipa TRT Afrika takwimu zake za mazao tangu mradi wa ngano uanze.

Kupanda aina ya ngano iliyoimarishwa kulimaanisha uvunaji ulifanyika mara mbili, sehemu fulani ya ardhi ilifanyiwa umwagiliaji wa maji huku nyingine ikiachwa ili kupitia msimu wa asili wa uzalishaji wa ngano.

Katika mwaka 2022/23 Ethiopia ilizalisha tani milioni 15.1 za ngano.

"Katika mwaka wa fedha wa 2022/23 kilimo cha ngano nchini Ethiopia kilifanyika katika hekta milioni 4.18. Kati ya hizi hekta milioni 1.33 zilikuwa ngano kutoka kwa mradi wa umwagiliaji maji wakati hekta milioni 2.85 zilivunwa wakati wa msimu mwingine," Bilene Seyoum msemaji wa ofisi ya Waziri Mkuu wa Ethiopia anaiambia TRT Afrika.

Seyoum anaongeza kuwa kufikia mwaka 2023/24, tani milioni 23 za ngano zilizalishwa, na kiasi cha ardhi inayolimwa kiliongezwa hadi hekta milioni 6.58.

"Kati ya hizi hekta milioni 2.97 zilitengwa kwa ajili ya ngano inayozalishwa chini ya kilimo cha umwagiliaji, wakati hekta milioni 3.61 zilizalishwa katika misimu mingine ya kawaida ya uzalishaji wa ngano."

Takwimu kutoka wizara ya kilimo ya Ethiopia zinaonesha kuwa takriban wakulima milioni 3.4 walihusika katika uzalishaji wa ngano ya umwagiliaji mwaka 2023/24, ambayo Seyoum anasema "inaonesha uwekezaji mkubwa katika eneo hili."

Seyoum anaiambia TRT Afrika kuwa katika mwaka wa 2024/2025 nchi inapanga kupanua ardhi kwa ajili ya uzalishaji wa ngano hadi hekta milioni 8.37.

"Kati ya hizi hekta milioni 4.27 zitakuwa chini ya umwagiliaji wakati hekta milioni 4.1 zitaachwa kwa uzalishaji wa kawaida wa ngano kulingana na msimu wa asili," anafafanua.

Kusawazisha kujitosheleza na mahitaji ya watu.

Wakati nchi inajitahidi kujitosheleza kwa uzalishaji wa kilimo pia inakabiliwa na changamoto za hali mbaya kwa watu.

Shirika la Mpango wa Chakula Duniani, WFP limesema Ethiopia imekuwa "mojawapo ya maeneo yenye njaa duniani inayotokana na mizozo, watu kuhama makazi yao na hali mbaya ya hewa."

Ethiopia inasema kufikia mwaka 2023/24, tani milioni 23 za ngano zilizalishwa/ Picha:Ofisi Waziri mkuu wa Ethiopia 

"Jumla ya watu milioni 5.5, kati yao milioni 1.7 ni wakimbizi wa ndani, wana tatizo kubwa la njaa," WFP imesema katika taarifa kwenye tovuti yake.

Inasema "inahitaji dola za Kimarekani milioni 338 kwa haraka ili kuendelea kutoa msaada kwa watu walio hatarini zaidi wa Ethiopia, hadi Mei 2025."

Hili limeonekana kukatiza tangazo la nchi hiyo juu ya kujitosheleza kwa ngano, lakini ofisi ya Waziri Mkuu wa Ethiopia imetetea lengo lake kama lile la kuongeza uzalishaji wa chakula cha ndani.

“Tunaposema Ethiopia inajitosheleza kwa ngano, tunamaanisha kuwa nchi hiyo haitegemei tena uagizaji wa ngano kutoka nje kutokana na ongezeko kubwa la uzalishaji wa ndani katika miaka ya hivi karibuni. Kama matokeo, hitaji la kuagiza ngano kutoka nje limeondolewa," ofisi ya Waziri Mkuu wa Ethiopia ilisema katika taarifa.

"Ethiopia haiagizi tena ngano kutoka nje," inasisitiza.

Ofisi ya Waziri Mkuu inakiri kwamba ingawa kutafuta kujitosheleza kwa ngano na kwa ujumla uzalishaji wa chakula ni njia "ngumu na yenye changamoto", kuna mafanikio ambayo imedhamiria kufikia na kudumisha.

TRT Afrika