Eritrea: Kwa nini tulijiunga tena na mamlaka ya kikanda ya IGAD baada ya miaka 16

Eritrea: Kwa nini tulijiunga tena na mamlaka ya kikanda ya IGAD baada ya miaka 16

Eritrea inasema inataka kuchangia tena katika maendeleo na kukuza amani na usalama wa kikanda
Eritrea ilijiondoa kutoka shirika la IGAD mwaka 2007 lakini sasa imeamua kurudi  / Photo: AFP

Eritrea imejiunga tena na Mamlaka ya Maendeleo ya Kiserikali (IGAD), takriban miaka 16 baada ya kujiondoa kwenye chombo hicho, anasema waziri wa habari Yemane Meskel.

"Eritrea ilianza tena shughuli zake katika IGAD na kuchukua kiti chake" katika mkutano ulioandaliwa na jumuiya hiyo ya mataifa saba nchini Djibouti siku ya Jumatatu, Meskel alisema kwenye Twitter.

Alisema nchi iko tayari kufanya kazi kuendeleza "amani, utulivu na ushirikiano wa kikanda."

Rais wa Eritrea Isaias Afwerki aliwaambia waandishi wa habari wakati wa ziara yake nchini Kenya mwezi Februari kwamba nchi yake itaungana tena na IGAD "kwa wazo la kufufua shirika hili la kikanda."

Mzozo wa mipaka

Katika taarifa yake rasmi kwa mkutano wa IGAD Jumatano, Workeneh Gebeyehu, katibu mtendaji wa IGAD, alipongeza kurejea kwa Eritrea katika shirika hilo,

"Nichukue fursa hii kukaribisha tena Eritrea kwa familia ya IGAD," alisema.

Eritrea ililisimamisha uanachama wake katika IGAD mwaka wa 2007 kufuatia kutofautiana kwa maswala na nchi zingine wanachama .

Sababu zilikuwa pamoja na shirika la IGAD kuitaka Kenya kutatua mzozo wa mpaka kati ya Ethiopia na Eritrea wakati huo.

Eritrea ilijitenga na Ethiopia mwaka 1993 na kupigana vita vya mpaka vya miaka miwili na jirani yake ambavyo vilihatarisha uhusiano hadi makubaliano ya amani kati yao kufanyika mwaka 2018.

Isaias mwenye umri ya miaka 77, hakuhudhuria mkutano wa wa Jumatatu wa IGAD nchini Djibouti, aliwakilishwa na waziri wa mambo ya nje Osman Saleh na mshauri wa rais Yemane Ghebreab.

TRT Afrika na mashirika ya habari