Mawasiliano ya Rais Erdogan yanaashiria nia mpya ya kurekebisha uhusiano uliodorora na Marekani katika miaka ya hivi karibuni kutokana na tofauti / Picha: Reuters Maktaba.

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan alizungumza kwa njia ya simu na Rais mteule wa Marekani Donald Trump kufuatia ushindi wake katika uchaguzi, akimpongeza na kueleza matumaini ya kuimarishwa kwa ushirikiano kati ya Uturuki na Marekani katika miaka ijayo.

Katika maongezi hayo ya Alhamisi, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Urais wa Uturuki kupitia X, Erdogan aliwasilisha heri yake ya muhula mpya wenye matunda katika uhusiano wa Marekani- Uturuki, akisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa nchi mbili katika masuala ya kikanda na kimataifa.

Huku Mashariki ya Kati ikikabiliwa na changamoto kubwa, kuanzia maeneo ya migogoro inayoendelea hadi shinikizo la kiuchumi, Erdogan alisisitiza uwezekano wa ushirikiano kati ya nchi hizo mbili ili kuchangia utulivu na kushughulikia masuala muhimu ya usalama.

Mazungumzo ya kiongozi wa Uturuki yanaashiria nia mpya ya kurekebisha uhusiano uliodorora katika miaka ya hivi karibuni kutokana na tofauti kuhusu sera za Syria, ushirikiano wa kijeshi na mizozo ya kidiplomasia.

Kama washirika wa NATO, Marekani na Uturuki zina uhusiano wa muda mrefu wa ulinzi na biashara lakini zimekabiliwa na mvutano kuhusu sera za Mashariki ya Kati za Washington, kama vile msaada wa Marekani kwa kundi la kigaidi la YPG nchini Syria.

Ankara pia imeikosoa Washington kwa kukosa ushirikiano dhidi ya shirika la kigaidi la FETO, ambalo kiongozi wake alifariki huko Pennsylvania mwezi uliopita.

Majadiliano ya Erdogan na Trump yanaangazia nia ya pamoja ya viongozi hao wawili katika kuweka upya mwelekeo wa uhusiano kati ya Marekani na Uturuki, huku mataifa yote mawili yakichukua nafasi muhimu katika kudhibiti migogoro katika Mashariki ya Kati na kushughulikia masuala mapana zaidi, kama vile mgogoro wa wakimbizi na juhudi za kukabiliana na ugaidi.

Waangalizi wanaona ushirikiano huu kama fursa kwa Uturuki na Marekani kukuza maslahi ya pande zote, kuashiria uwezekano wa kupata uwiano wa karibu zaidi wa vipaumbele vya kimkakati vya kikanda.

TRT Afrika