Rais wa Rwanda Paul Kagame amemteua tena Édouard Ngirente kama Waziri Mkuu wa nchi hiyo, ofisi ya rais nchini Rwanda ilitangaza.
Uteuzi huo umekuja siku chache baada ya Kagame kuapishwa kuitumikia nchi hiyo kwa mihula mingine mitano.
Ngirente, ambaye kitaaluma ni mchumi, aliteuliwa kwa mara ya kwanza kuhudumu katika nafasi hiyo kwa mara ya kwanza Agosti 2017.
"Najisikia fahari sana kuteuliwa tena kuwa Waziri Mkuu," alisema Ngirente kupitia ukurasa wake wa X, pia akimshukuru Rais Paul Kagame, akisisitiza dhamira yake ya kuitumikia nchi hiyo.
Uteuzi wa Mawaziri na wajumbe wengine ndani ya nchi hiyo hufuata mashauriano kati ya Rais na Waziri Mkuu wa Rwanda.
Edouard Ngirente ni nani?
Mtaalamu huyo wa uchumu anakuwa Waziri Mkuu wa 11 nchini Rwanda baada ya nchi hiyo kupata uhuru mwaka 1962 na wa sita baada ya Mauaji ya Kimbari ya 1994 dhidi ya Watutsi.
Alizaliwa katika Wilaya ya Gakenke, Mkoa wa Kaskazini, mwaka wa 1973.
Kabla ya uteuzi wake mwaka 2017, Ngirente alifanya kazi Benki ya Dunia huko nchini Marekani akiwa amejiunga na taasisi hiyo kama mshauri wa Mkurugenzi Mtendaji anayesimamia nchi 20 za Afrika, kabla ya kupandishwa cheo na kuwa mshauri mkuu mwaka 2017.
Kabla ya hapo, Ngirente amewahi kushika nyadhifa za juu katika Wizara ya Fedha na Mipango ya Kiuchumi nchini Rwanda.
Ana Shahada ya Uzamivu katika Uchumi wa Kilimo kutoka Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Louvain (UCL) nchini Ubelgiji.
Pia ana digrii mbili za baada ya kuhitimu, moja katika Usimamizi wa Hatari za Kifedha kutoka kwa Facultés Universitaires Saint-Louis ya Brussels na nyingine katika Uchumi wa Kilimo kutoka UCL.
Pata habari zaidi kupitia Whatsapp channels