mental health

Huku dunia ikiadhimisha siku ya afya ya akili , shirika la afya duniani linasema kuwa kuna ongezeko la visa vya watu wenye matatizo ya afya ya akili.

"Mmoja kati ya watu wanane duniani wanaishi na matatizo ya afya ya akili," katibu mkuu wa Shirika la Afya Duniani Tedros Adhanom amesema, " lakini, watu wengi sana hawawezi kupata huduma bora ya afya ya akili."

Afya ya akili ni hali ya ustawi wa kiakili ambayo huwawezesha watu kukabiliana na hali ya maisha, kutambua uwezo wao, kujifunza vizuri na kufanya kazi vizuri, na kuchangia katika jamii yao.

Wataalam wa afya wanasema mambo ya kibinafsi ya kisaikolojia na ya kibaolojia, matumizi ya madawa ya kulevya na unasaba vinaweza kuwafanya watu kuwa katika hatari zaidi ya matatizo ya afya ya akili.

"Tunataka afya ya akili ipewe heshima kama mojawapo ya haki za kibinadamu," Tedros om ameongezea.

Afya ya akili barani Afrika

Hali mbaya za kijamii, kiuchumi, kijiografia na kimazingira - ikijumuisha umaskini, vurugu, ukosefu wa usawa na kunyimwa mazingira salama- pia huongeza hatari ya watu kukumbwa na hali ya afya ya akili.

Barani Afrika vurugu katika sehemu tofauti zimechangia watu kuwa na matatizo ya afya ya kiakili huku mamilioni wakilazimika kuhama makwao na wengine kuwa wakimbizi.

Shirika la Afya duniani linasema katika kanda ya Afrika, zaidi ya watu milioni 116 wanakadiriwa kuishi na tatizo la afya ya akili, wengine kwasababu ya majanga, na wakati mwingine kuhusishwa na vitendo vya kishirikina kama vile uchawi.

TRT Afrika