Viwango vilivyotolewa na Shirikisho hilo Aprili 4, DRC imeshika nafasi ya 63 duniani na 12 barani Afrika kwa ubora wa mchezo huo unaopendwa na kufuatiliwa zaidi duniani, na hivyo kuibuka kidedea katika ukanda wa Afrika Mashariki. Picha:/Getty

Na Edward Qorro

TRT Afrika, Istanbul, Uturuki

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ndiye kinara wa soka kwa ukanda wa Afrika Mashariki, kulingana na Shirikisho la vyama vya mpira wa miguu duniani (FIFA).

Viwango vilivyotolewa na Shirikisho hilo Aprili 4, DRC imeshika nafasi ya 63 duniani na 12 barani Afrika kwa ubora wa mchezo huo unaopendwa na kufuatiliwa zaidi duniani, na hivyo kuibuka kidedea katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Chui hao kutoka DRC walishika nafasi ya nne katika makala ya 34 ya michuano ya AFCON 2023 yaliyofanyika nchini Ivory Coast.

Kwa kushika nafasi ya 92 duniani, Uganda inakuwa ya pili kwa ubora wa Soka katika ukanda wa Afrika Mashariki, ikifuatiwa na Kenya, ambayo imechupa nafasi nne juu, na kuwa ya 107 duniani.

Hivi karibuni, kikosi cha 'Harambee Stars', kilitwaa ubingwa wa mashindano ya mataifa manne dhidi ya Mashujaa wa Zimbabwe, katika mchezo wa Fainali uliofanyika katika uwanja wa Bingu, mjini Lilongwe nchini Malawi.

Nafasi ya nne kwa ubora wa soka katika ukanda wa Afrika Mashariki inakwenda kwa Tanzania, ambaye imesalia katika nafasi ya 119 duniani, licha ya kuifunga Mongolia hivi karibuni.

Kama ilivyo kwa DRC, 'Taifa Stars' nayo ilishiriki michuano ya AFCON 2023. Hata hivyo, Tanzania ilikuwa ya mwisho kwenye msimamo wa kundi F, baada ya kuambulia alama mbili kwenye mashindano hayo makubwa na yenye hadhi barani Afrika.

Rwanda ni ya tano kwa ubora ikiwa na alama 131, baada ya kupanda juu kwa nafasi mbili, ikifuatiwa na Burundi ambayo ipo katika nafasi ya 140 duniani, wakati Sudan ya Kusini inashika mkia ikiwa ni ya 167.

TRT Afrika