Maandamano yalizuka mjini Kinshasa dhidi ya balozi za kidiplomasia na baadhi ya mashirika ya kimataifa siku ya Jumamosi, huku vijana wenye hasira wakichoma magari kadhaa ya baadhi ya balozi na Umoja wa Mataifa.
Waandamanaji hao waliishutumu jumuiya ya kimataifa kwa "kutojali" katika kukabiliana na mzozo wa usalama na kibinadamu mashariki mwa DR Congo.
Serikali ililaani vitendo vya unyanyasaji na kuwataka raia kuwa watulivu katika taarifa yake kufuatia mkutano wa dharura wa usalama ulioitishwa na Waziri wa Mambo ya Ndani Peter Kazadi.
"Rais wa Jamhuri (Felix Tshisekedi) anasema kwamba ingawa tunaelewa baadhi ya kero za wenzetu na kile kinachotokea mashariki mwa nchi, hatua za waandamanaji zinakiuka vifungu kadhaa vya sheria za kimataifa," taarifa hiyo ilisema.
Imetangaza kufanya uchunguzi, huku serikali ikisema imeimarisha usalama katika balozi nchini.
MONUSCO kujitoa
Bintou Keita, mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa Kudhibiti Utulivu nchini DRC (MONUSCO) pia alilaani mashambulizi dhidi ya wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa, akisisitiza kwamba "magari kadhaa" yalichomwa wakati wa maandamano.
Alizitaka mamlaka za mahakama za Kongo kuanzisha uchunguzi kwa nia ya kuwafungulia mashtaka wahusika.
MONUSCO, ambayo imetumwa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo tangu 1999, itaanza kujiondoa taratibu kutoka eneo hilo mwezi Aprili.
Maelfu ya watu katika majimbo mawili ya mashariki yaliyoathiriwa zaidi na migogoro ya Kivu Kaskazini na Ituri wanaishi katika kambi.
Msururu wa maandamano umezuka nchini DR Congo dhidi ya kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa, ambacho watu wanakituhumu kwa kushindwa kuzuia ghasia za makundi mengi yenye silaha.