Connie Chiume ni mwigizaji aliyeshinda tuzo nyingi. /Picha: Chiume/Instagram

Na

Charles Mgbolu

Raia wa Afrika Kusini wanaenzi urithi wa muigizaji mkongwe Connie Chiume, aliyefariki Jumanne mjini Johannesburg akiwa na umri wa miaka 72.

Familia yake, katika taarifa, ilisema alikufa hospitalini na kuomba wapewe "faragha katika kipindi hiki kigumu."

Raia wa Afrika Kusini wameshtushwa na taarifa hio, huku serikali ya Afrika Kusini ikiongoza kutoa rambirambi katika mitandao ya kijamii.

"Tunatuma salamu zetu za dhati kwa familia, marafiki, na wafanyakazi wenza wa mshindi wa tuzo nyingi na mwigizaji nguli Connie Chiume. Kazi yake nzuri itakumbukwa kila wakati, "serikali iliandika kwenye mtandao wa X.

Kazi ya uigizaji iliyong'aa

Chiume ni maarufu kwa nafasi yake katika filamu za kimataifa kama vile Black Panther na Disney's Lion King, pamoja na flamu za ndani kama vile Zone 14 na Gomora.

Televisheni ya Black Entertainment BET ilimtaja kama "ikoni wa kweli."

“#BET inamkumbuka Muigizaji Nguli na Mwanaharakati wa Sanaa wa Afrika Kusini Connie Chiume. Ikoni wa kweli ambayo sanaa na talanta yake iligusa wengi, kazi yako ya kipekee katika tasnia yetu imeunda urithi wa kudumu," kituo hicho kiliandika kwenye mtandao wa X. Familia ya Chiume haijafichua hali iliyosababisha kifo chake lakini imeahidi "kuwasiliana na maelezo zaidi" baadaye.

Black Panther

Katika filamu ya Black Panther ya 2018, Chiume aliigiza kama Zawavari, mwanachama wa Baraza la Kikabila la Wakandan.

Katika muendelezo wa 2022 Black Panther: Wakanda Forever, alipangwa kuchukua nafasi ya Zuri (Forest Whitaker) kama Mzee Statesman wa Wakanda.

Amepokea tuzo nyingi, pamoja na Tuzo ya Filamu na Televisheni ya Afrika Kusini (SAFTA).

Ameacha watoto wanne, wa kiume wawili na binti wawili.

TRT Afrika