'' Unaweza kuwa na shahada ya chuo kikuu lakini usiwe na talanta ya uongozi.'' Ndio maneno ya Millie Bulungu, mwalimu mstaafu.
Sokomoko imeibuka kati ya chama cha kitaifa cha walimu nchini Kenya KNUT, na jopo lililoteuliwa kufanyia mabadiliko sekta ya elimu baada ya jopo hilo kupendekeza kuwa walimu wakuu wa shule za msingi wasio na shahada washushwe vyeo.
Lakini wazo hili limetajwa kuwa la kudhalilisha na chama cha walimu kusema kuwa watalipinga kwa njia zote.
"Tumejipanga, na tunataka kung'ata pale inapobidi ili walimu wetu wabaki vizuri kama walivyokuwa.'' amesema katibu mkuu wa KNUT Collins Oyuu. ''Ikiwa chochote, baadhi ya walimu hawa ni miongoni mwa wafanyakazi bora zaidi ushawahi kuona.'' aliongoeza.
Kwa upande wake, mwalimu mstaafu Millie Bulungu ameambia TRT Afrika, '' Nimekuwa mwalimu kwa zaidi ya miaka 30, na nimeona shule nyingi zikiongozwa na watu wenye shahada ila wanafanya vibaya sana.''
Mafunzo ya ziada
Mwalimu Millie, ambaye kufikia kustaafu alikuwa amepanda cheo kuwa naibu wa mwalimu mkuu, anapendekeza kuwa badala ya kuwashusha walimu wakuu walioko kazi, ni bora wapewe fursa ya kujiendeleza kimasomo na wahifadhi nafasi zao.
'' Nakumbuka wakati wetu tulikuwa tunaandaliwa warsha za mara kwa mara ili kujiimarisha zaidi na kuwekwa sawa na mabadiliko yanayokuja ya kiteknolojia na mitaala,'' ameambia TRT Afrika.
Mapendekezo ya mabadiliko
Katibu mkuu wa chama cha Walimu, Collins Oyuu, aliambia wanahabari kuwa, wanaungamkono mabadiliko katika sekta ya elimu lakini sio yale yanayowaponza walimu.
Kwa mujibu wa KNUT, zaidi ya 90% ya walimu hao wamehitimu vyuo vikuu, na wanapendekeza wale wengine wapewe fursa ya kurudi chuoni kuongeza shahada.
Jopo lilipendekeza walimu wanaosimamia shule za msingi, chini ya mfumo mpya wa CBC waendelee kushikilia nyadhifa hadi Disemba 2023 ambapo mabadiliko yangefanywa.
Ilipendekeza kuundwa kwa shule za pamoja, ambazo zitajumuisha chekechea, shule ya msingi na sekondari chini ya mwavuli mmoja na kusimamiwa na mwalimu mkuu mmoja.
Pia ilipendekeza walimu wakuu wasiokuwa na shahada watatafutiwa nafasi zingine za chini za kufanya kazi.
Kuna zaidi ya shule 23,000 za msingi zilizoidhinishwa na wizara ya elimu kuandaa mfumo mpya wa mtaala wa JSS huku baadhi zikisimamiwa na wakuu wa shule wasiohitimu vyuo.
Chama cha walimu KNUT kimesema kitawasilisha mapendekezo mbele ya tume ya kuwaajiri walimu kitaifa ili kufanyia marekebisho mfumo wa mishahara kuendana na mabadiliko katika sekta ya elimu.
Bi Millie, kwa ushauri wake ameitaka serikali iendelee kuwakagua walimu katika kazi zao, na kutumia maelezo hayo kuwapa vyeo.
''Mwalimu hapandishwi cheo kwa sababu ya shahada zake, bali kwa sababu ya umahiri wake kazini,'' ameambia TRT Afrika. '' Ila naomba walete wakaguzi waliokuwa wakifuatilia kazi zetu darasani na kuangalia nidhamu na matokeo kwani ndivyo vigezo vyema vya kumpandisha mwalimu cheo.'' aliongeza.