Chad imesitisha makubaliano na Ufaransa ambayo awali yalikuwa na lengo la kuimarisha ushirikiano katika usalama na ulinzi kati ya mataifa hayo mawili.
"Serikali ya Jamhuri ya Chad inatoa maoni ya kitaifa na kimataifa kuhusu uamuzi wake wa kusitisha mkataba wa ushirikiano wa kiulinzi uliotiwa saini na Jamhuri ya Ufaransa," ilisema taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje siku ya Alhamisi.
Taarifa hiyo, iliyotiwa saini na Waziri wa Mambo ya Nje Abderaman Koulamallah, ilisema kwamba baada ya miongo kadhaa ya uhuru, ni wakati wa nchi hiyo "kuthibitisha mamlaka yake kamili na kufafanua upya ushirikiano wake wa kimkakati kulingana na vipaumbele vya kitaifa."
Ilisema uamuzi wa kusitisha mkataba huo, ambao ulirekebishwa Septemba 2019, hauonyeshi kwa vyovyote kuzorota kwa uhusiano wa kihistoria na uhusiano wa urafiki kati ya mataifa hayo mawili.
Mazungumzo rasmi
Chad kwa sasa inaongozwa na Mahamat Idriss Deby aliyeapishwa kama rais wa Chad Mei 2024, baada ya miaka mitatu ya kuongoza kwa muda chini ya utawala wa kijeshi katika nchi hiyo.
Chad inasema "imesalia na nia ya kudumisha uhusiano wenye kujenga na Ufaransa katika maeneo mengine yenye maslahi ya pamoja, kwa manufaa ya mataifa yote mawili."
Mamlaka iliahidi kuheshimu taratibu zilizowekwa katika vifungu vya makubaliano, ikiwa ni pamoja na muda wa notisi, na kushirikiana na mamlaka ya Ufaransa ili kuhakikisha mabadiliko hayo yanafanyika kwa wepesi.
Uamuzi huo ulitangazwa wakati Waziri wa Ufaransa wa Ulaya na Mambo ya Nje Jean-Noel Barrot alipotembelea nchi hiyo ya Afrika Magharibi.
Barrot, ambaye aliwasili katika mji mkuu wa N'Djamena siku ya Jumatano, alifanya mazungumzo na Rais wa Chad Mahamat Idriss Deby siku ya Alhamisi.
Mzozo wa Sudan
Majadiliano yao yalilenga hasa vita vya Sudan, hali ya dharura ya kibinadamu mashariki mwa Chad iliyotokana na wimbi la wakimbizi wa Sudan wanaokimbia vita, na matarajio ya ushirikiano wa pande mbili, ofisi ya rais ilisema katika taarifa yake.
Chad inaungana na nchi nyingine za Sahel zikiwemo Niger na Mali katika kukomesha ushirikiano wa kiusalama na kiulinzi na mtawala wao wa zamani.
Mnamo Agosti 2023 baada ya kuondolewa madarakani kwa rais mteule Mohamed Bazoum, viongozi wa kijeshi wa Niger walitangaza kufuta makubaliano ya kijeshi na Ufaransa.
Hii ilikuja baada ya uongozi wa kijeshi ya Mali mwaka 2022 kutangaza uamuzi sawa wa kujiondoa kutoka kwa makubaliano ya ulinzi na Ufaransa.