Wanajeshi wa Burundi chini ya kikosi cha AUSSOM / Picha: Reuters

Burundi haitakuwa tena sehemu ya Kikosi cha Kusaidia na Kuleta Utulivu wa Umoja wa Afrika nchini Somalia (AUSSOM).

Ujumbe mpya wa AUSSOM uliopitishwa wa kusaidia amani nchini Somalia uliidhinishwa na baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kupitia Azimio nambari 2767 (2024) na unatazamiwa kuanza kutekelezwa tarehe 1 Januari 2025.

AUSSOM inachukua nafasi ya Kikosi cha Mpito cha Umoja wa Afrika nchini Somalia (ATMIS) ambacho kilichukua nafasi ya Kikosi cha Umoja wa Afrika nchini Somalia (AMISOM) kuanzia tarehe 1 Aprili 2022.

" Kutokana na hali zote, Burundi inalazimika kuondoka—kwa sababu ambazo sijui," balozi wa zamani wa Burundi kwa Umoja wa Afrika, Alaine Nyamitwe amesema katika nakala aliyoandika.

Burundi imekuwa na zaidi ya wanajeshi 3,000 katika oparesheni hiyo Somalia ambayo ndiyo kubwa zaidi ya amani ya Umoja wa Afrika.

Barua ambayo imeandikwa na Somalia kwa waziri wa usalama wa taifa wa serikali ya Burundi inaashiria kuwa Somalia imekubali ombi la Burundi kuondoa majeshi wake.

"Wizara ya ulinzi inazingatia barua yako, tunakushukuru kwa majibu yako kwa wakati na kwa kusisitiza msimamo wa Jamhuri ya Burundi kuhusu suala hili. Huku tukisikitika kuwa muafaka haukuweza kufikiwa kuhusu ugawaji wa askari wa vikosi vya ulinzi vya Burundi tunakubali uamuzi wako na tunatazamia kukubali kutoshiriki kwa AUSSOM, " barua ya kutoka kwa waziri wa usalama wa Somalia Abdulkadir Mohamed Nur imesema.

" Maendeleo haya yanastahili tafakari, kwani yanaashiria mwisho wa safari ya miaka 17 ya Burundi nchini Somalia," Nyamitwe amesema.

Kujiondoa kwa wanajeshi wa Burundi kuna maana gani?

"Katika mazingira ya pande nyingi kama vile shughuli za usaidizi wa amani, maafikiano ndio kanuni kuu—hasa katika suala la mshikadau wa muda mrefu," Nyamitwe ameongezea.

Chini ya kikosi cha ATMIS kitengo cha kijeshi kilipangwa kuwa na wanajeshi 18, 586 hadi tarehe 31 Desemba 2022 na kisha kupunguza maafisa 2,000.

Wanajeshi zaidi walipangwa kuondoka nchini Somalia ifikapo Septemba 2023 na baadaye Juni 2024 na kuelekea kuondoka kwa mwisho mnamo Desemba 2024.

Kikosi cha ATMIS kinasema upungufu huo utazingatia hali ya usalama iliyopo nchini Somalia na utaongozwa na tathmini za pamoja za kiufundi za mara kwa mara.

TRT Afrika