Bunge ya Kenya imemhoji Dorcas Agik Oduor aliyeteuliwa na Rais William Ruto kuwa mwanasheria mkuu.
Rais William Ruto alitengua baraza lake la mawaziri Juni 2024 pamoja na mwanasheria mkuu baada ya maandamano nchini humo yaliyoongozwa na Gen Z yakimtaka abadilishe safu ya uongozi wake.
Oduor alihojiwa na kamati ya bunge inayoongozwa na Spika wa bunge Moses Wetangula.
" Tuambie nini ungechukulia kuwa maoni yako ya ofisi ya mwanasheria mkuu," Naibu spika wa bunge Gladys Boss alimuuliza.
" Tunahitaji kuangalia upya makosa ya watu ili tupunguze wale wenye makosa madogo madogo gerezani .Wengi wa waliokuwa chini ya ulinzi walikuwa vijana na walikuwa maskini. Je, pesa taslimu ndiyo njia pekee ya kupata haki?" alijibu.
Oduor aliulizwa na wabunge kwa nini serikali hushindwa kesi mahakamani na kupata hasara.
" Inawezekana kwamba una kesi mbaya, utaipoteza. Inaweza kuwa una uwakilishi mbaya au usiofaa. Unaweza kupoteza kesi kwa sababu nyingine yoyote, hakuna kati ya zilizo hapo juu," Oduor ameelezea.
" Iwapo nitashindwa itakuwa jukumu langu kama mkuu wa sheria kuangalia upya kesi kabla hazijaanza kuhakikisha ni thabiti ili tusipate hasara. Pia itakuwa kazi yangu kushauri Wizara na MDAS jinsi ya kushughulikia masuala ya mahakama," Oduor ameelezea.
Mbunge Junet Mohamed alimuuliza swali kuhusu historia yake ya kazi.
" Umejaribu mara kadhaa kuwa jaji lakini umepuuzwa sifa zako za kitaaluma, unaweza kutuambia kwa nini, Tume ya Huduma ya sheria , JSC ilikupa sababu?
" Kuhusu JSC, naamini haukuwa wakati wangu na si mimi pekee ambaye sikufanikiwa, hawatoi sababu za kukukataa," alimjibu.
Mwanasheria Mkuu aliyeteuliwa Dorcas Oduor ametangaza thamani yake kuwa Sh85 milioni ( zaidi ya $657,640) zikijumuisha sehemu za ardhi, nyumba na gari.
Iwapo ataidhinishwa, atachukua nafasi ya Justin Muturi ambaye sasa ni Katibu wa Baraza la Mawaziri la Utumishi wa Umma.
Oduor aliongezea kuwa akiidhinishwa, atakuwa Mwanasheria Mkuu msikivu na wakili wa watu wa Kenya.