Rais Ruto alitengua baraza lake lote la mawaziri Julai 2024 kufuatia maandamano ya Gen Z, ambayo pia yalimshinikiza kubadilisha uongozi nchini humo.
Kamati ya Bunge inayoratibu zoezi hilo, inaoongozwa na Spika wa Bunge hilo, Moses Wetangula.
Kwa upande wake, Dkt Andrew Karanja amejitetea kuwa ataleta mabadiliko iwapo atapewa fursa ya kushika hatamu ya Wizara ya Kilimo.
" Ukithibitishwa, mtawashughulikia vipi wauza sukari, wanalindwa na watu wachache wenye tamaa, na tunajua hivi vikundi navyo vinazorotesha mageuzi katika sekta ya sukari," Mbunge Mishi Mboko alimuuliza Dkt Karanja.
" Tuna upungufu wa sukari na hapo ndipo tatizo linapoanzia, tani 300 hivi, makampuni ya biashara yanastawi wakati uzalishaji haukidhi mahitaji yetu," Dkt, Karanja alijibu.
" Tunahitaji kuziba pengo ili tuweze kusimamia sukari nyingi inayoingia nchini. Tutangeneza mchakato wa uagizwaji wa bidhaa hiyo na kuhakikisha kuwa kuna ushindani na uwazi katika sekta."
Naye spika wa bunge hilo, alipata fursa ya kumuuliza mteule huyo.
" Wakulima wetu wa mahindi ni wachapakazi sana, wanateseka wakizalisha kidogo na wanateseka zaidi wakizalisha zaidi, utafanya nini katika suala la wakulima wa mahindi na nafaka nchini?" alihoji Spika Wetangula.
" Tunajua mhusika mkuu ni Bodi ya Taifa ya Nafaka na Mazao (NCPB) na Wasagaji," alijibu Karanja.
" Hili ni eneo ambalo serikali imeingilia kati kutoa rasilimali lakini linapokuja suala la kufaidika kuna changamoto . Ni eneo ambalo ni gumu kwa sababu wakati bei zinapoongezeka watumiaji pia wana shida, inahitaji umakini wa hali ya juu," Dkt Karanja alijibu.
" Najua kushughulika na makampuni ya biashara haramu ni suala kubwa, lakini iwapo nikiidhinishwa na kamati hii, ninatoa taarifa kwa makampuni. Watakuwa nje ya biashara. Moja ya kanuni ninazothamini sana ni uadilifu. Nitawashughulikia," alijitetea Karanja.
Awamu ya aliyekuwa Waziri wa Kilimo Mithika Linturi, ilitawaliwa na tuhuma za ufisadi katika sekta tofauti, ikiwemo uwepo wa mbolea feki iliyosambazwa kwa wakulima.