Mwanasiasa kutoka kambi ya upinzani nchini Uganda Dkt. Kiiza Besigye amefunguliwa mashtaka katika Mahakama ya Kijeshi mjini Kampala.
Ameshtakiwa kwa makosa yanayohusiana na usalama na kumiliki silaha kinyume cha sheria.
Besigye amekana mashtaka hayo.
Hasimu huyo wa kisiasa wa Rais Yoweri Museveni wa Uganda inadaiwa alichukuliwa kwa nguvu akiwa jijini Nairobi, Kenya wiki iliyopita na kurudishwa Uganda.
Mashtaka kulingana na mahakama ya kijeshi
Upande wa mashtaka unadai kuwa Dkt. Kiiza Besigye, Haji Obed Lutale na wengine ambao hawakua mahakamani, kati ya Oktoba 2023 na Novemba 2024 wakiwa Geneva Switzerland, Athens Ugiriki na Nairobi Kenya walifanya mikutano yenye nia ya kutafuta usaidizi wa aina tofauti na kulenga maeneo ya kijeshi nchini Uganda wakiwa na nia ya kugandamiza usalama wa majeshi.
Pia wameshtakiwa kuwa na silaha kinyume na sheria.
Upande wa mashtaka umedai kuwa Dkt. Kiiza Besigye, Hajji Obed Lutale mnamo tarehe 16 Novemba 2024 wakiwa katika eneo la makazi la Riverside Apartments Nairobi Kenya, walipatikana kinyume na sheria wakiwa na bastola na risasi ambazo kwa kawaida hutumika pekee na wanajeshi.
Hivi sasa wawili hao watasalia rumande katika Magereza ya Luzira hadi Disemba 2, 2024.