Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wakiwa katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York / Picha: Reuters

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeidhinisha ujumbe wa Umoja wa Afrika wa kuleta utulivu na msaada nchini Somalia - unaojulikana kama AUSSOM - siku ya Ijumaa ambao utachukua nafasi ya operesheni kubwa ya AU ya kupambana na ugaidi kuanzia Januari 1, 2025.

Baraza hilo lenye wanachama 15 lilipitisha rasimu ya azimio lililoongozwa na Uingereza kwa kura 14 za ndio, Marekani ilijizuia kupiga kura.

AUSSOM itachukua nafasi ya Kikosi cha Mpito cha Umoja wa Afrika nchini Somalia (ATMIS), ambacho mamlaka yake yatakamilika Desemba 31.

Rasimu ya maandishi inawaruhusu wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) kupeleka hadi wafanyakazi 12,626 waliovalia sare, wakiwemo polisi 1,040, kwa AUSSOM hadi tarehe 30 Juni 2025, na kukamilisha kufikia tarehe hii upangaji upya wa wanajeshi wote wa AU kutoka ATMIS hadi AUSSOM.

Balozi James Kariuki, naibu mwakilishi wa kudumu wa Uingereza katika Umoja wa Mataifa, alisema azimio hili "kwa nguvu" linaimarisha uungwaji mkono wa Baraza kwa Somalia.

"Inaidhinisha AUSSOM kuunga mkono Somalia katika mapambano yake dhidi ya Al-Shabaab, kuimarisha juhudi za kuleta utulivu wa Somalia, na kuwezesha utoaji wa usaidizi wa kibinadamu," Kariuki alisema.

Somalia na Ethiopia zote zilishiriki katika kikao hicho. Nchi hizo zimekuwa katika mzozo tangu Ethiopia ilipofikia makubaliano mwezi Januari na eneo lililojitenga la Somalia la Somaliland kutumia bandari yake ya Bahari Nyekundu ya Berbera. Uturuki imekuwa ikifanya kazi kutatua mivutano hii.

Azimio la Ankara lilitiwa saini tarehe 12 Disemba, ambalo pia liliendeshwa na Uturuki liliashiria mabadiliko katika uhusiano kati ya majirani wa Pembe ya Afrika.

Katika taarifa ya pamoja, viongozi wa Somalia na Ethiopia wamesisitiza kwamba Azimio la Ankara "lilithibitisha tena heshima, umoja, uhuru na haki kamili ya eneo."

TRT Afrika