Waziri wa Fedha wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba aliwasilisha Hotuba ya Bajeti Kuu ya Serikali, ambapo Serikali imeliomba Bunge kuidhinisha bajeti ya zaidi ya dola bilioni 18.7 (shilingi trilioni 49.35) kwa mwaka 2024/25.
Hotuba ya Bajeti imependekeza kusamehe kampuni za usindikaji chai kutoka kwa malipo ya AMT kwa muda wa miaka mitatu. Lengo la hatua hii ni kupunguza sekta ya chai ambayo kwa sasa inashuka kwa bei ya soko.
Pia imeomba kufanywa marekebisho ya kodi inayolipwa na watu binafsi wanaohusika na usafirishaji wa abiria kwa magari yanayobeba abiria kati ya 16 hadi 25 hadi dola 248 (TZS 650,000) kutoka dola 210 (TZS 550,000).
Bajeti pia imelenga kitengo cha dijitali. Inapendekeza kutoza Kodi ya zuio kwa kiwango cha asilimia 5 kwenye malipo ya biashara ya kutengeneza maudhui ya kidijitali (digital content creators) yanayofanywa na wakaazi (resident business).
Lengo lake ni kuongeza wigo wa kodi na kuzingatia kanuni za usawa za utozaji wa kodi. Hatua hii inatarajia kuongezamapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 968.
Kuna pendekezo la kuanzishwa kwa ushuru wa zuio wa 5% kwa malipo yanayofanywa na wakaazi na wasio wakaazi kwa waundaji wa maudhui ya kidijitali ambao ni wakazi wa Tanzania.
Waziri amesema hakutakuwa na Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa kiwango cha asilimia 0 kwenye madini ya dhahabu yatakayouzwa kwa Benki Kuu ya Tanzania.
Lengo kuu ni kuhamasisha uuzaji wa dhahabu kwa Benki Kuu ya Tanzania, na hivyo kuongeza akiba ya nchi ya fedha za kigeni na kupunguza tatizo la uhaba wa dola za Marekani.Aidha, hatua hii inalenga pia kuchochea ukuaji wa viwanda vya kusafisha madini (refineries) nchini kwa kuwa Benki Kuu ya Tanzania hununua dhahabu baada ya kusafishwa na viwanda hivyo pekee.
Ushuru kuondolewa
Ushuru utaondolewa katika magari, vifaa, mitambo na bidhaa nyingine kwa matumizi rasmi ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania hatua itakayowezesha Jeshi kutekeleza majukumu yake ya kuilinda nchi.
Ndege, injini ya ndege, sehemu za ndege na matengenezo ya ndege kwa mtengenezaji wa ndani wa anga, kuunganisha au uzalishaji itaondolewa ushuru. Hii itakuwa pamoja na msamaha wa ushuru unaotolewa kwa anayetoa huduma ya usafiri wa ndege na wa anga.
Sekta ya michezo pia imenufaika hasa kandanda.
Kuna msamaha wa Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye uingizwaji wa vifaa vya kiteknolojia kwa ajili ya kuwasaidia waamuzi (Video Assistant Referee equipment and accessories).
Hii inalenga kuhakikisha kuwa nchi inapata vifaa muhimu vya michezo ikizingatiwa kuwa Tanzania itakuwa wenyeji wa AFCON mwaka 2027 ambayo nchi hiyo inatazamia kuhodhi michuano ya AFCON itakuja na manufaa mbalimbali kwa nchi kama kuongezeka kwa akiba ya fedha za kigeni, kukuza taswira ya nchi.
Ushuru pia umetolewa kwa madini ya thamani, na vito vingine vya thamani kwenye viwanda vya kusafishia madini , ikiwa na lengo la kuongeza mchango wa sekta ya madini katika Pato la Taifa.
Ushuru mpya
Bajeti ya Tanzania ya Mawka 2024/2025 imependekeza kuweka ushuru upya kwa bidhaa na huduma kadhaa.
Bajeti inataka kutoza shilingi 382 kwa kila kilo ya gesi asilia inayotumika kwenye magari. Hii ina lengo la kuongeza mapato yatakayotumika katika kufanya matengenezo ya barabara pamoja na kuleta usawa kwa kuwa magari yanayotumia mafuta tayari yanachangia mapato kwa ajili ya matengenezo ya miundombinu ya barabara.
Mapato yatakayotokana na chanzo hiki yatapelekwa Mfuko wa Barabara.
Imependekeza kutoza Ushuru wa Bidhaa kwa kiwango cha Shilingi 500 kwa kilo moja ya rangi za mafuta (solvent based paints and vanishes) zinazotoka nje ya nchi.
Lengo lake serikali inasema, ni kuongeza mapato ya Serikali na kupata fedha za fidia ya athari hasi zinazotokana na matumizi ya bidhaa hizo.
Pia imependekeza kutoza Ushuru wa Bidhaa kwa kiwango cha Shilingi 300 kwa kilo ya tomato sauce na tomato ketchup, pamoja na chilli sauce na chilli ketchup zile zinazotoka nje ya nchi.
Serikali imesema lengo lake ni kuongeza mapato ya Serikali na kupata fedha za fidia ya athari hasi zinazotokana na matumizi ya sukari na chumvi iliyopo katika bidhaa hizo. Hatua hii inatarajia kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 634.
Kuna pendekezo pia ya kutoza Ushuru wa Bidhaa kwa kiwango cha asilimia 10 kwenye thamani ya dau la kamari (value of the stake on betting) kwenye Michezo ya Kubahatisha na Bahati Nasibu ya Taifa.
Mapato yatakayokusanywa kutoka chanzo hiki ni kwa ajili ya kugharamia bima ya afya kwa watu wasio na uwezo na makundi maalum hususan wanawake wajawazito na watoto wa umri chini ya miaka mitano.
Ushuru inaongezwa katika vileo tofauti. Ushuru wa bidhaa kwa kiwango cha dola 2.7 (Tshilingi 7,000) utatozwa kwa kila lita ya 'Un-denatured Ethyl Alcohol' yenye kilevi cha asilimia 80 au zaidi inayotoka nje ya nchi, na dola 1.9 (Tshilingi 5,000) kwa kila lita ya 'Un-denatured Ethyl Alcohol' yenye kilevi cha asilimia 80 au zaidi inayozalishwa ndani ya nchi.
Utozaji huo hautahusisha 'Un-denatured Ethyl Alcohol' inayotumika kwa matumizi mengine yasiyohusu uzalishaji wa vilevi baada ya kupata ridhaa ya Waziri mwenye dhamana ya masuala husika. Aidha, viwango tofauti vinapendekezwa kwa lengo la kulinda viwanda vya ndani.
Ushuru kupunguzwa
Bajeti imepoendekeza kupunguza Ushuru wa Bidhaa kutoka shilingi 63.80 kwa lita hadi shilingi 56 kwa lita ya maji ya kunywa yaliyosindikwa kwenye chupa inayozalishwa nchini.