Na Coletta Wanjohi
TRT Afrika, Istanbul, Uturuki
Huku Joe Biden akiamua kutogombea tena urais nchini Marekani, maswali yanayoibuka ni ipi hatma ya makubaliano yake na Afrika?
Uongozi wa Joe Biden ulionekana kufufua mahusianao makubwa kati ya Afrika na Marekani ambayo yalionekana kudidimia wakati wa Donald Trump alipokuwa rais.
Utawala wake ulitoa ahadi ya kuwekeza dola bilioni 55 barani Afrika kwa miaka mitatu kuanzia 2022.
Marekani iliukaribisha Umoja wa Afrika kama mwanachama wa kudumu wa G20, kupanua ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji, kuwekeza vikubwa katika usalama wa chakula na afya, na kuzindua mpango wa mabadiliko ya kidijitali.
Rais Biden alifanya mkutano wake wa kwanza na viongozi wa Afrika Disemba 2022.
"Mafanikio na ustawi wa Afrika ni muhimu ili kuhakikisha maisha bora ya baadaye kwa sisi sote, sio tu kwa Afrika," rais Biden alisema.
Uhusiano wa Rais Biden na Kenya
Kenya ni kati ya nchi zilizonufaika kwa kiwango kikubwa kutoka uongozi wa Joe Biden. Rais William Ruto amekuwa rais wa pekee barani Afrika kualikwa katika ziara rasmi nchini Marekani baada ya miaka 15 tangu kualikuwa kwa rais yoyote mwengine.
Biden aliiangazia Kenya kama mpatanishi mkubwa barani katika migogoro ya DRC, Sudan na pia kati ya Somalia na Ethiopia. Biden pia ameendeleza umuhimu wa Kenya katika mapambano dhidi ya wanamgambo wa Al Shabaab.
Rais Ruto alikubali ombi la uongozi wa Marekani kutuma maafisa wa polisi 1000 nchini Haiti kuleta amani katika nchi inayosumbuliwa na magenge ya wahalifu, na Kenya ikapata dola milioni 300 kutoka Marekani.
Zaidi ya haya, Kenya itapokea dola milioni 40 kwa ajili ya mpango wa demokrasia, haki za binadamu na utawala bora nchini Kenya.
Ushirikiano wa dola milioni 7 kuimarisha Huduma ya Kitaifa ya Polisi wa Kenya bila kusahau mpango wa dola milioni 2.2 katika sekta ya magereza.
Biden pia aliahidi dola milioni 4.9 katika ufadhili mpya kwa Kenya na nchi nyingine za Afrika Mashariki ili kuboresha ushirikiano katika kupambana na uhalifu mitandaoni na kuwawajibisha wahalifu.
Kenya pia imetengewa kupokea dola milioni 1.5 katika kuimarisha Tume ya Uchaguzi.
Sekta ya ulinzi nchini Kenya nayo imenufaika kutoka kwa rais Biden. Kwa mara ya kwanza, wanajeshi wa Kenya wameanza mafunzo katika shule ya kijeshi ya Marekani.
Septemba mwaka huu, Kenya imepanga kupokea takribani magari 150 ya kijeshi kutoka Marekani.
Kenya itapokea helikopta 16 za kijeshi na Marekani itaboresha Uwanja wa Ndege wa Manda Bay katika pwani ya Kenya kwa kuongeza urefu ili kuboresha operesheni dhidi ya kundi la kigaidi la al-Shabaab.
Rais Biden aliitambua Kenya kama mshirika mkuu ambae siye mwanachama wa NATO, nafasi ya kifahari.
Haya na mengineyo, ni ishara tosha kwamba Rais Joe biden alijenga uhusiano madhubuti na Kenya, uhusiano ambao ulitarajiwa kuimarika zaidi iwapo Biden angerudi katika muhula wake wa pili.
Swali ni je, utekelezaji wa makubaliano haya utaendelea bila kuwepo kwa Biden? Kwani kila rais anaingia na vipaumbele vyake na mipango mipya ya sera za kigeni.