Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat ameomba DRC na Rwanda kufanya maafikiano/ Picha: Wengine

Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat amesema kuwa anasikitishwa sana na mvutano unaoendelea Mashariki mwa DRC akihofia kuwa hali ya usalama inaedelea kudorora kwa kasi.

"Ninatoa wito kwa viongozi wa eneo hilo, haswa wale wa DRC na Rwanda kuzingatia kufanya mazungumzo ndani ya mifumo miwili ya Kiafrika inayoongozwa na rais Joâo Lorenzo wa Jamhuri ya Angola na rais wa zamani wa Kenya Uhuru Kenyatta, " Faki amesema katika taarifa yake.

DRC na Rwanda zinazozana huku DRC ikiishutumu Rwanda kwa madai ya kuunga mkono waasi wa M23 ambao ni tishio kwa usalama DRC, lakini Rwand siku zote imekuwa ikikana tuhuma hizo.

Faki amesema kuwa ni muhimu kwa viongozi wa Rwanda na DRC kutafuta njia ya kusuluhisha mizozo ya kisiasa bila kujali asili yao " katika roho ya ushirikiano wa kindugu."

Kiongozi huyo wa Tume ya Umoja wa Afrika amesema ni muhimu utulivu wa mataifa yote katika eneo lazima uhakikishwe na maisha ya raia yalindwe kikamilifu.

Pia ametoa wito kwa mataifa yote ya kigeni kujiepusha kabisa na uingiliaji wowote wa masuala ya ndani ya nchi zote za Afrika, hasa zile za Maziwa Makuu ya Afrika.

TRT Afrika