Na Coletta Wanjohi
Istanbul, Uturuki
Kwa miaka 15 sasa Rachel Anekea amekuwa mshonaji wa nguo jijini Nairobi, akikuza biashara yake polepole.
Wateja wake wangempata kila mara katika Jumba la Mall ya Sunbeam kwenye Mtaa wa Mfangano katika mji mkuu wa Kenya Nairobi, ambapo alikuwa na duka lake. Alikua anamiliki cherehani tatu kukuza biashara yake.
Walakini miaka kadhaa ya kazi ngumu kwa mama wa mtoto mmoja, ilisombwa mnamo Juni 25, 2024, wakati watu wasiojulikana waliposhambulia na kuharibu jengo lao.
"Ilikuwa siku ya maandamano ya kupinga kodi, yakiongozwa na watoto wetu wadogo ambao wana sababu ya kweli," Anekea anaelezea TRT Afrika.
"Hata nilienda mitaani siku hiyo kuwa sehemu ya historia kubwa, hata hivyo, hatukujua kuwa jengo letu lingeshambuliwa," anasema.
Anekea anasema kundi la watu walitaka kuingia kwa nguvu kwenye jengo ambalo limefungwa kwa usalama kwa sababu ya maandamano.
"Walinzi walipokataa kuwaruhusu kuingia walikwenda na kurudi wakiwa na hasira nyingi, walitumia nguvu na hata kumwaga petroli katika jengo hilo kabla ya kuliteketeza," anaeleza kwa sauti ya kutetemeka.
Machozi yakaanza kumtoka haraka.
“Nilipoteza mashine zangu zote, na nguo ambazo wateja walikuwa wameagiza. Takriban familia 600 ambazo zilitegemea biashara katika jengo hilo kujipatia riziki hazina chochote sasa. Sina chochote,” anasema huku akiwa na huzuni.
Anekea anasema kando na kupotea kwa mali, wana kiwewe kwa sababu baadhi ya wapangaji wenzao walikufa katika mapigano hayo.
"Wawili walichomwa mle ndani, mmoja alikufa wakati akijaribu kuruka kutoka kwenye jengo lililoungua na wengine wengi kupata majeraha, hizi ni nyakati za huzuni sana maishani mwetu," aeleza.
Ripoti ya polisi imesema kuwa mwili wa pili uliokotwa kutoka kwenye jengo hilo tarehe 2 Juni 2024, ukiwa umeungua vibaya na kuharibika.
Anekea ni miongoni mwa maelfu ya wengine wanaohesabu hasara za kimwili na kiakili kutoka sehemu mbalimbali za nchi, wamekuwa wahanga wa kile wanachosema ni wahalifu walioteka nyara maandamano hayo ya amani.
Duka kuu liitwalo Quickmart katika barabara hiyo hiyo katika jengo la Anekea liliporwa, huku lingine liitwalo Naivas kwenye barabara ya Moi Avenue katika wilaya kuu za biashara zikiwa zimeunganishwa pia.
Tawi la Carrefour Supermarket, shirika la kimataifa la rejareja na uuzaji jumla la Ufaransa kwenye Mtaa wa Wabera mkabala na City Hall lilisalia na rafu tupu pia. Uharibifu wa aina hiyohiyo ulishuhudiwa katika maeneo mengine ya nchi.
Katika jiji hilo hilo David Murage, dereva wa teksi, ana wasiwasi kuhusu mkopo aliochukua mwezi uliopita kutoka kwa benki.
"Nilipochukua mkopo kuendeleza biashara yangu ya teksi, matarajio yalionekana kuwa mazuri kwa sababu tunaingia katika kipindi cha kuingia kwa watalii wa kigeni. Ni wakati wetu wa kupata pesa nzuri, kwa hivyo nilinunua gari lingine ili kuhudumia wateja ambao nilikuwa nimepata” Murage aliieleza TRT Afrika.
“Nina wasiwasi sasa kwa sababu baadhi ya watalii kutoka nje ya nchi waliokuwa tayari wamepanga kutumia huduma yangu kwa muda wa miezi miwili kuanzia Agosti hadi Septemba wamenighairi, wamesema wana hofu baada ya kuangalia maandamano ya wiki tatu kwenye vyombo vya habari, ” anaeleza.
Sasa inabidi afikirie njia mbadala za kuongeza mapato na kuhudumia mkopo wake.
Ni nani aliyesababisha uharibifu huo?
Rais William Ruto katika mazungumzo ya rais na baadhi ya wanahabari nchini Kenya alisema mbali na kupoteza maisha, mali imeharibiwa.
"Mali ya thamani ya zaidi ya $18.6 milioni (Kshs 2.4 bilioni) imeharibiwa. Ofisi ya Jaji Mkuu imechomwa moto, Jengo la Kaunti ya Nairobi limechomwa, na bunge limechomwa. Hii ndio hali,” Rais William Ruto aliambia wanahabari tarehe 30 Juni 2024.
Maandamano ya kupinga muswada wa sheria ya fedha yaliongozwa na vijana, maarufu kama Gen Z na yaliwekwa alama juu ya amani na yalilenga ajenda, ambayo ilikuwa ya kwanza kukataa Mswada wa Fedha wa 2024, kisha kumtaka rais asitie saini.
"Tuna amani" ni sehemu ya nyimbo ambazo vijana walipiga kelele huku wakikumbana na ugomvi na jeshi la polisi mara kwa mara. Hakuna uharibifu ulioripotiwa wakati maandamano ya amani yalipofanyika tarehe 18 Juni 2024, siku ya kwanza ya maandamano ya mitaani katika sehemu za nchi.
Tarehe 25 Juni baadaye katika siku ambayo bunge lilivamiwa na sehemu za majengo yake kuchomwa moto pamoja na majengo mengine ikiwa ni pamoja na pale Anekea alikuwa na duka.
Zaidi ya watu 20 wameripotiwa kufariki katika makabiliano na polisi siku hiyo na kwa jumla Shirika la Haki za Kibinadamu la Kenya limeweka idadi ya waliouawa kuwa takriban 39.
Mnamo Juni 26, Rais William Ruto alitangaza kwamba hatotia saini mswada wa Fedha akiomba uondolewe.
Siku iliyofuata bado watu waliingia mitaani na safari hii wengine wakamtaka ajiuzulu.
Lakini siku iyo hiyo ndipo uharibifu wa wazi uliposhuhudiwa huku mali zaidi ikishambuliwa na kuharibiwa na kusababisha hasara zaidi, hasa katika jiji kuu la Nairobi.
Kiongozi wa muungano wa upinzani, Azimio, Raila Odinga alikosoa kile alichokiita utekaji nyara wa maandamano ya amani ya vijana na wahalifu.
"Matukio ya watu wakipora uharibifu na kuiba yalikuwa tofauti kabisa na yale yaliyoshuhudiwa mwanzoni mwa maandamano wakati "Gen Z" walikuwa wakidhibiti kikamilifu mchakato na mipango yake,"
Aliishutumu serikali kwa kuwafahamu wahuni hao na kuwataka polisi kuwakamata.
Gumzo lililofanywa na vijana kwenye mtandao wa Space X mnamo tarehe 2 Julai 2024, lililaumu uharibifu huo kwa wahalifu, huku baadhi ya vijana wakidai kuwa wahalifu hao wamepewa rushwa kwa wingi na kuilaumu serikali kwa kupanga uporaji huo ili kudharau maandamano yao ya amani dhidi ya serikali ya William Ruto.
Hata hivyo, serikali kwa upande mwingine pia imejitokeza kukemea uharibifu huo ikiapa kuwakamata waliofanya hivyo.
Kurugenzi ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai, DCI, hata iliweka picha za watu wanaoshukiwa kuwa sehemu ya wahalifu hao na kuomba usaidizi wa umma kuwatambua wengine.
"Katika uchunguzi unaoendelea kuhusu uvunjaji na uteketezaji wa maduka makubwa ya Chieni huko Nyeri na Nanyuki, polisi katika kaunti ya Nyeri na Laikipia wamepata bidhaa nyingi zilizoibwa na kuwakamata washukiwa kadhaa."
DCI iliandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa X mnamo tarehe 4 Julai 2024, ikionyesha picha za washukiwa walionaswa na kamera.
Nini kinafuata?
Sekta zingine na watu binafsi bado hawajatangaza ni kiasi gani cha hasara walichokipata kutokana na maandamano hayo kwa njia ya moja au nyengine.
Waandamanaji hawakurejea barabarani tarehe 4 Julai kama walivyopanga, huku vijana wengi wakiwasiliana kupitia mitandao ya kijamii juu ya haja ya kupanga mambo upya.
Wengine walisema juhudi zao zinaonekana kuhatarishwa na watu waliolipwa, hivyo haja ya kupanga upya hatua nyingine ya amani dhidi ya serikali na sera zake.
Lakini kwa wengi kama Rachel Anakea ambao biashara zao ziliharibiwa mpango wa kurekebisha upya ni mbaya.
Ana wasiwasi kuhusu jinsi ya kuelezea wateja ambao tayari walikuwa wameagiza na kulipa kwamba alipoteza kazi yake baada ya kuchomwa kwa biashara yake.
Hajui ni jinsi gani atafufua juhudi za miaka 15 ambazo ziliteketezwa na watu ambao anaamini hawakushiriki katika maandamano ya amani ya iliongozwa na vijana wa kupinga muswada wa fedha.
Hana bima ya biashara yake ambayo anasema ilikuwa na thamani ya takriban dola 2000.
"Sisi ni wafanyabiashara wadogo, hatufikirii masuala ya bima, sikuwa na yoyote. Na ningejuaje kwamba ningepoteza mali yangu kupitia uharibifu?" anaeleza.
“Mmiliki wa jengo hilo yamkini ameliwekea bima jengo lake, lakini hapokei hata simu zetu. Polepole ninapoteza akili yangu kwa sababu sasa niko kwa wasaria wema, sina kitu tena na hakuna wa kumtegemea,” anasema.