Sudan iliongeza muda wa kufungwa kwa anga ya nchi hiyo hadi Julai 31 huku mapigano yakiendelea kati ya jeshi na kundi la wanamgambo la Rapid Support Forces (RSF).
Katika taarifa, Mamlaka ya Usafiri wa Anga ya Sudan ilisema Jumatatu, kuwa anga ya Sudan itasalia kufungwa kwa safari zote za ndege hadi Julai 31.
Ni misaada ya kibinadamu tu na safari za ndege za uokoaji ambazo zitaruhusiwa.
Sudan imeathiriwa na mapigano kati ya jeshi la Sudan na Rapid Support Forces tangu Aprili, katika mzozo uliosababisha vifo vya zaidi ya raia 3,000 na kujeruhi maelfu, kulingana na madakitari nchini Sudan.
Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) linakadiria kuwa karibu watu milioni tatu wamekimbia makazi yao kwa ajili ya huu mzozo wa sasa nchini Sudan.
Mikataba kadhaa ya kusitisha mapigano iliyosimamiwa na wapatanishi wa Saudia na Marekani kati ya wapinzani hao wanaozozana imeshindwa kumaliza ghasia nchini humo.