Kundi la kigaidi la Al-Shabaab limevamia hoteli moja katika mji mkuu wa Somalia Mogadishu siku ya Alhamisi. Kulikuwa na milipuko kadhaa ya mabomu na milio ya risasi.
Mapigano kati ya vikosi vya usalama na washambuliaji yalizuka kufuatia shambulizi katika Hoteli maarufu ya SYL, ambayo iko karibu na ikulu ya rais.
Watu wengi walijeruhiwa, akiwemo Msemaji wa Serikali Farhan Jimale, waandishi wa habari na wabunge kadhaa.
Al-Shabaab imefanya mashambulizi kadhaa nchini Somalia hivi karibuni.
Ripoti za vyombo vya habari nchini zilisema baadhi ya wabunge waliuawa katika tukio hilo.
Serikali bado haijatoa tamko kuhusu shambulio hilo. Al-Shabaab walidai kuhusika na shambulizi kwenye chaneli yake ya Telegram huku milio ya risasi ikiendelea kusikika karibu na hoteli hiyo.
Hoteli hiyo, iliyoko katika eneo lenye ngome, hutumiwa mara kwa mara na maafisa wa serikali kwa mikutano.