Mahakama ya Ubelgiji imemhukumu kiongozi wa zamani wa wanamgambo wa Rwanda kifungo cha maisha jela kwa mauaji kadhaa na ubakaji uliofanywa wakati wa mauaji ya kimbari ya 1994.
Seraphin Twarhirwa, 66, alipatikana na hatia ya kushiriki moja kwa moja au kusimamia ukatili huo na wanamgambo wa Hutu Interahamwe mjini Kigali wakati wa mauaji ya Watutsi na Wahutu wenye msimamo wa wastani miaka 30 iliyopita.
Mshtakiwa wa pili Pierre Basabose, mshirika wa karibu wa rais wa zamani Juvenal Habyarimana, pia alipatikana na hatia ya "mauaji ya kimbari" na "uhalifu wa kivita" kwa kufadhili wanamgambo.
Lakini mzee huyo mwenye umri wa miaka 76, ambaye anaugua ugonjwa wa shida ya akili na hakuweza kuhudhuria vikao vya kesi, hakuhukumiwa kifungo gerezani kwa sababu za kiafya.
Twarhirwa na Basabose walikana mashtaka hayo wakati wa kusikizwa kesi yao kwa miezi miwili huku mawakili wao wakisema kwamba watakata rufaa.
Kesi dhidi ya wanaume hao wawili, ambao walikamatwa 2020 nchini Ubelgiji ambapo walikuwa wakiishi uhamishoni, ilikuwa ya sita kufanyika nchini humo kuhusiana na mauaji ya kimbari nchini Rwanda mnamo 1994.
Uamuzi huo ulikaribishwa na Michele Hirsch, mwanasheria aliyewawakilisha waathiriwa katika kesi hiyo.
Ubelgiji ilitawala Rwanda wakati wa ukoloni na ina idadi kubwa ya watu wa Rwanda wanaoishi nje ya nchi.
Inakadiriwa Watutsi 800,000 na Wahutu wenye msimamo wa kadiri waliuawa wakati wa siku 100 za mauaji ya halaiki yaliyosababishwa na kushambuliwa kwa ndege ya Habyarimana mnamo Aprili 6, 1994.
Hukumu hiyo ya Ubelgiji inajiri siku chache baada ya mahakama nchi jirani ya Ufaransa Jumatano kumfunga gerezani daktari wa zamani Sosthene Munyemana kwa miaka 24 kwa kuhusika katika mauaji ya kimbari.