Uganda inaomboleza mwanariadha wake Rebecca Cheptegei ambaye amefariki mapema akiwa katika Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Moi mjini Eldoret nchini Kenya ambapo alikuwa amelazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU).
Mwanariadha huyo wa mbio za marathon mwenye umri wa miaka 33, alishiriki katika Michezo ya Olimpiki ya hivi majuzi ya Paris.
Mpenzi wake Dickson Ndiema Marangach anatuhumiwa kuingia bila taarifa siku ya Jumapili nyumbani kwa Cheptegei akiwa na mtungi wa lita tano za petroli. Taarifa zinasema, Cheptegei alikuwa kanisani na watoto, na aliporudi, ndipo alipomiminiwa mafuta na kuchomwa.
Kaimu Mkurugenzi wa MTRH Dkt Owen Menach alithibitisha kufariki jana usiku baada ya viungo vyake vyote kuharibika.
"Kwa bahati mbaya, tulimpoteza baada ya viungo vyake vyote vya mwili kuharibika jana usiku," alisema Kaimu Mkurugenzi wa MTRH Dkt Owen Menach. Amesema hospitali itatoa ripoti kamili kuhusu suala hilo baadaye mchana,
"Tuna huzuni kubwa kutangaza kifo cha mwanariadha wetu, Rebecca Cheptegei mapema asubuhi ya leo ambaye alifanyiwa ukatili wa nyumbani. Kama Shirikisho, tunalaani vitendo hivyo na tunataka haki itendeke," Muungano wa Wanariadha ya Uganda imesema katika akaunti yake ya X.
Kenya imetoa rambi rambi zake kwa kifo cha mwanariadha huo kutoka Uganda Rebecca Cheptegei.
"Kwa niaba ya #TeamKenya tunatuma rambirambi zetu kwa jumuiya ya michezo ya Uganda, familia, na marafiki wa Rebecca Cheptegei. Kipaji cha Rebecca, na uvumilivu kama bingwa wa kushikillia rekodi ya Uganda ya Marathon ya Wanawake na Mwana Olimpiki wa Paris 2024 daima itakumbukwa na kusherehekewa," @olympicsKenya imesema katika akaunti yake ya X.
"Kifo chake kisichotarajiwa na cha kusikitisha ni msiba mkubwa, na mawazo na sala zetu ziko pamoja nawe wakati huu mgumu tunapoheshimu urithi wake na kutetea kukomeshwa kwa unyanyasaji wa kijinsia," uongoiz huo wa wanariadha nchini Kenya umeongezea.
Mvutano wa muda
Madaktari wanasema Cheptegei alipata asilimia 80 ya majeraha ya moto baada ya mpenzi wake anayedaiwa kumwagia mwili wake na petroli na kumchoma moto.
Mpenzi huyo Dickson Ndiema Marangach pia alipata majeraha ya moto wakati wa shambulio hilo. Pia alilazwa katika kituo hicho cha ICU na takriban asilimia 30 ya majeraha ya moto.
Baba yake mwanariadha huyo Mzee Joseph Cheptegei alifafanua kuwa wawili hao walikuwa marafiki tu kwa muda.
Alidai kuwa walikuwa wakizozana kuhusu ardhi yake huko Endebes, Trans Nzoia ambapo shambulio hilo lilitokea.
Baba huyo alisema wawili hao walikuwa na kesi iliyokuwa ikichunguzwa na DCI.
Alisema mwanariadha huyo ana watoto wawili ambao baba yao ni mtu tofauti anayeishi Uganda.
Mzee Cheptegei alisema wawili hao walikuwa wametengana kwa muda mrefu lakini Jumapili Marangach aliingia kinyemela hadi nyumbani ambapo alianzisha mashambulizi.