Afrika Kusini imeelezea "wasiwasi mkubwa" kwa uamuzi wa Rais wa Marekani Donald Trump kusimamisha misaada ya kifedha kwa nchi hiyo.
Wizara ya mambo ya nje ya nchi hiyo ilisema hatua hiyo haina "usahihi wa ukweli" na inashindwa kutambua historia ya Afrika Kusini ya ubaguzi wa rangi.
Rais Trump alitia saini amri ya utendaji siku ya Ijumaa akinukuu sheria mpya ya Afrika Kusini ya unyakuzi wa ardhi na kesi yake ya mauaji ya kimbari dhidi ya Israel katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ), Ikulu ya White House ilitangaza.
Afrika Kusini ilisema hatua ya Trump inaonekana kama kampeni ya "taarifa potofu na propaganda" dhidi ya nchi hiyo, wizara yake ya mambo ya nje ilisema katika taarifa yake.
Wakimbizi wa Afrikana
"Inasikitisha kuona kwamba masimulizi kama haya yanaonekana kupata upendeleo miongoni mwa watoa maamuzi nchini Marekani," iliongeza.
Umiliki wa ardhi ni suala lenye utata nchini Afrika Kusini, huku mashamba mengi yakiwa bado yanamilikiwa na watu weupe miongo mitatu baada ya kumalizika kwa ubaguzi wa rangi na serikali ilikuwa chini ya shinikizo kutekeleza mageuzi.
Agizo la Trump linajumuisha kipengele cha kusaidia "wakimbizi wa Kiafrikana wanaoepuka ubaguzi wa rangi unaofadhiliwa na serikali."
Lakini Afrika Kusini ilisema "inashangaza kwamba amri ya kiutendaji inatoa nafasi ya hadhi ya ukimbizi nchini Marekani kwa kundi nchini Afrika Kusini ambalo limesalia kuwa miongoni mwa watu walio na fursa kubwa kiuchumi," kulingana na taarifa ya wizara ya mambo ya nje.
Nchi hiyo ni mshirika mkubwa wa kibiashara wa Marekani barani Afrika. Marekani ilitoa msaada wa karibu dola milioni 440 kwa Afrika Kusini mwaka 2023, kulingana na data rasmi ya Marekani.
Suluhu za kidiplomasia
Wizara ya mambo ya nje ya Afrika Kusini imesema bado imejitolea kutafuta suluhu za kidiplomasia kwa kutoelewana au mizozo yoyote.
Rais Cyril Ramaphosa hajazungumzia mzozo huo wa hivi punde wa kidiplomasia lakini hapo awali ametetea sheria hiyo mpya, akisema haihusiani na unyakuzi wa ardhi.