Maafisa 19 wa kaunti ya Migori wajiuzulu kwa sababu ya vyeti ghushi. /Picha: Migori County Assembly (Facebook)

Katibu wa Kaunti ya Migori Oscar Olima alisema, amepokea barua ya kujiuzulu kutoka kwa wafanyakazi 19 ambao wanadaiwa kumiliki vyeti feki, maafisa hao wameamua kuacha kazi wenyewe kabla ya kuwachukulia hatua na kaunti, huku wengine wakiomba fursa ya kujitetea.

Katibu huyo alisema pia wanawachunguza wafanyakazi zaidi wa kaunti hio, walio na vyeti vya kutiliwa shaka katika msako unaoendelea wa kusaka vyeti ghushi za masomo.

Olima pia alidokeza ya kwamba hatua hiyo imechukuliwa kufuatia ripoti ya ukaguzi iliyoandaliwa na Taasisi ya Ukaguzi wa Rasilimali Watu mnamo 2023 na ripoti ya hesabu ya wafanyakazi iliyofanywa na serikali ya kaunti.

Olima alisema wafanyakazi wote 93 wa kaunti walioghushi vyeti vya masomo wameondolewa kwenye orodha ya mishahara. Huku wengine wamepewa fursa ya kujieleza.

Hapo awali, Naibu Rais wa Kenya Rigathi Gachagua ametoa suluhu kwa rais wa Kenya William Ruto namna ya kupunguza fungu la mshahara.

Amesema iwapo wataanza kuchunguza maafisa wanaofanya kazi serikalini bila vyeti halali, huenda wakapata watu elfu kumi na hatimaye kupunguza fungu la mshahara wa watu wanaolipwa pesa hizo.

Amenukuliwa akisema hivyo pindi alipokuwa katika kongomano la tatu la fungu la mshahara mjini Nairobi katika jengo la Bomas Kenya.

Vilevile, amedokeza kwamba Rais pekee ndie anayeweza kuongoza mchakato huo, kwa vile maafisa wengi waliokaribu naye huenda wakawa ndio wahusika wakuu.

TRT Afrika