Mamlaka ya Nigeria ilisema lori hilo lilikuwa limejaa kupita kiasi lilipoanguka katika jimbo la kaskazini la Kano mnamo Julai 1, 2024. / Picha: Reuters

Takriban watu 25 wamefariki na wengine 53 kujeruhiwa baada ya lori kuanguka katika jimbo la kaskazini la Kano siku ya Jumatatu, mamlaka ilisema.

Ofisa wa usalama barabarani wa Jimbo la Kano Ibrahim Abdullahi alisema uchunguzi wa awali ulionyesha dereva wa gari hilo alishindwa kulimudu na kusababisha kuacha barabara ya Kano-Zaria, barabara kuu inayounganisha Kano na jimbo jirani la Kaduna.

Abdullahi alisema ajali hiyo ilitokea mwendo wa saa tatu asubuhi kwa saa za huko (0200hrs GMT).

Askari wa usalama barabarani alisema lori lilikuwa limejaa kupita kiasi wakati ajali hiyo ilipotokea.

Kusafirisha mifugo

Gari hilo pia lilikuwa likisafirisha mifugo wakiwemo mbuzi na kondoo pamoja na nafaka.

"Madaktari walithibitisha kuwa wahasiriwa 25 waliuawa katika ajali hiyo," Abdullahi alisema, kama alivyonukuliwa na Redio inayomilikiwa na serikali Nigeria.

Abdullahi alionya dhidi ya kusafirisha binadamu na wanyama katika gari moja, akisema kitendo kama hicho kinakiuka kanuni za trafiki za Nigeria.

Wanyama kumi waliuawa katika ajali hiyo.

TRT Afrika