| Swahili
AFRIKA
2 dk kusoma
Sudan Kusini yaiomba Afrika Kusini msaada wa vifaa vya kupigia kura kuelekea uchaguzi Disemba 2026
Sudan inapanga kufanya Uchaguzi Mkuu Disemba 2026
Sudan Kusini yaiomba Afrika Kusini msaada wa vifaa vya  kupigia kura kuelekea uchaguzi Disemba 2026
Rais Salva Kirr wa Sudan Kusini alikutana na Rais Cyril Ramaphosa @PresidencyZA / Public domain
tokea masaa 8

Sudan Kusini imeiomba Afrika Kusini msaada wa kiufundi na vifaa vya kupigia kura ili kuhakikisha Uchaguzi wake Mkuu wa kwanza uliopangwa kufanyika Disemba 2026 unafanyika bila matatizo.

"Rais Kiir alisisitiza kwamba wakati Sudan Kusini imejitolea kuendeleza michakato yake ya kidemokrasia, nchi hiyo inahitaji usaidizi wa kiufundi na wa vifaa ili kuhakikisha mchakato mzuri katika uchaguzi ujao," kulingana na taarifa ya ofisi ya Rais wa Sudan Kusini kwenye mitandao ya kijamii. Mkutano kati ya viongozi hao wawili ulifanyika tarehe 19 Machi 2026, wakati wa ziara rasmi ya Rais Kiir nchini Afrika Kusini.

Ofisi ya Rais Kirr imesema majadiliano kati ya viongozi hao wawili wa nchi yalilenga uchaguzi ujao wa 2026, uungwaji mkono wa uchaguzi, na njia za kuboresha ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi hizo mbili.

"Rais Kiir alisisitiza kwamba msaada kutoka Afrika Kusini katika maeneo kama vile uchapishaji wa karatasi za kupigia kura na kutoa vifaa vya usajili wa wapigakura - utathaminiwa na Sudan Kusini," ofisi yake imeeleza.

"Wakati wa mkutano huo, Rais Kiir alisisitiza tena kwamba Sudan Kusini ina nia ya kufanya uchaguzi Disemba 2026. Alisisitiza kuwa Mkataba wa Amani Uliohuishwa unaendelea kuongoza uongozi wa mpito wa nchi na maandalizi ya uchaguzi yanaendelea. Alisema wazi kwamba serikali imedhamiria kusonga mbele na uchaguzi,” Ofisi yake ilifafanua.

Uchaguzi ulioahirishwa

Sudan Kusini haijawahi kuwa na Uchaguzi Mkuu tangu ilipopata uhuru wake mwaka 2011.

Mnamo Septemba 2024, serikali ya Sudan Kusini ilitangaza kuahirisha Uchaguzi Mkuu hadi Disemba 2026, kwa sababu ya ukosefu wa maandalizi.

Uchaguzi huo ulikuwa umepangwa kufanyika Disemba 2024.

Hii ilikuwa mara ya pili kwa nchi hiyo changa zaidi barani Afrika, kuahirisha uchaguzi na kuongeza muda wa mpito ulioanza Februari 2020.

Rais Salva Kiir na mpinzani wake wa zamani ambaye aligeuka kuwa naibu, Riek Machar, walitia saini makubaliano ya amani mwaka 2018 ambayo yalimaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka mitano na kusababisha vifo vya takriban watu 400,000, na njaa, na kuzalisha idadi kubwa ya wakimbizi.

Mnamo Machi 2025 Machar aliwekwa chini ya kifungo cha nyumbani na baadaye kuvuliwa wadhifa wake wa makamu wa rais na hatimae kushtakiwa kwa uhaini na uhalifu dhidi ya binadamu Septemba 2025.

CHANZO:TRT Swahili